Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Msumbiji kwa pamoja zimekubaliana kuendeleza na kudumisha ushirikiano katika masuala mbalimbali kupitia sekta za Ulinzi na Usalama kwa maslahi mapana na ustawi wa watu wao.
Akitoa taarifa ya majumuisho kwa Waandishi wa Habari, Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) amesema , Mkutano huo ni mwendelezo wa Ushirikiano mwema baina ya Tanzania na Msumbiji.
Mkutano huo, umewakutanisha wajumbe kutoka Wizara, Idara na Taasisi za kisekta kutoka nchi za Msumbiji na Tanzania, umeendeshwa katika mazingira ya kindugu, kirafiki na utulivu, ambayo yamewezesha majadiliano ya kina na hatimaye kufikia maazimio katika maeneo mbalimbali ya ushirikiano. Aidha, mkutano huo umeridhishwa na ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili na kusistiza umuhimu wa kuendeleza na kudumisha mashirikiano ya kudumu katika sekta za kimkakati zikiwemo za ulinzi na usalama, maliasili pamoja na mambo yahusuyo forodha.
Mkutano huo pia, umeridhishwa na utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Nne uliofanyika Mjini Maputo, Msumbiji kuanzia tarehe 27 – 29 Septemba, 2022. Licha utekelezaji kwa wakati, bado yapo baadhi ya maazimio yanaendelea kutekelezwa, kwa maana hiyo, Tume imeziomba nchi washirika, kuharakisha utekelezaji wa maazimio hayo.