Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Fedha na Mipango Zanzibar Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, akimkabidhi zawadi ya mlango uliotengenezwa kwa mbao za asili kutoka Zanzibar, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Uchumi na Fedha wa Korea Mhe. Kyungho Choo, baada ya kuhitimisha mazungumzo kati yao yaliyolenga kuimarisha ushirikiano, yaliyofanyika, Busan, Korea ya Kusini.
Mazungumzo yakiendelea wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, alipoongoza ujumbe wa Tanzania kuzungumza na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Uchumi na Fedha wa Korea Mhe. Kyungho Choo, kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano, yaliyofanyika, Busan, Korea ya Kusini.
Kamishna Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade, na Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje Bw. Melcksedeck Mbise (kushoto), wakifuatilia mazungumzo baina ya Tanzania na Korea, yaliyofanyika, Busan, Korea ya Kusini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Fedha na Mipango Zanzibar Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, akizungumza wakati Tanzania ilipokutana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Uchumi na Fedha wa Korea Mhe. Kyungho Choo, kujadiliana masuala ya mashirikiano, Busan, Korea ya Kusini.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Uchumi na Fedha wa Korea Mhe. Kyungho Choo, akizungumza wakati alipokutana na ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Fedha na Mipango Zanzibar Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, katika ukumbi wa hotel ya Ananti Hilton, Busan, Korea ya Kusini.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Busan, Korea Kusini)
Na. Saidina Msangi, WF, Busan, Korea.
Serikali ya Jamhuri ya Korea imeiwezesha Tanzania kupata mikopo yenye masharti nafuu kutoka Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Uchumi (EDCF) wa Korea yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni moja ili kugharamia miradi ya maendeleo katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2025.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Fedha na Mipango Zanzibar Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, alieongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano kati ya Korea na Afrika (KOAFEC) kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Uchumi na Fedha wa Korea Mhe. Kyungho Choo, pembezoni mwa Mkutano kati KOAFEC unaoendelea jijini Busan nchini Korea Kusini.
Alisema kuwa mikopo hiyo kutoka Korea imesaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali katika pande zote mbili za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na baadhi ya miradi iliyoidhinishiwa fedha mwezi Februari, 2023 ipo katika hatua mbalimbali za maandalizi.
‘‘Miradi iliyokatika hatua mbalimbali za utekelezaji ni pamoja na ujenzi wa hospitali ya rufaa ya Binguni inayotarajiwa kugharimu takriban dola za Marekani milioni 164, kuboresha hospitali ya Taifa ya Muhimbili dola milioni 227.3, ujenzi wa taasisi ya mafunzo dola milioni 75.8 na ujenzi wa taasisi ya teknolojia dola milioni 60, ujenzi wa kituo cha kisasa cha mafunzo ya reli dola milioni 75.8 na fedha nyingine zitaelekezwa katika sekta za nishati, uvuvi na fedha,’’alisema Mhe. Mkuya.
Alisema kuwa Tanzania ilipata mkopo wa masharti nafuu kutoka Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Uchumi (EDCF) kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Selander (Tanzanite Bridge) uliogharimu Dola za Marekani milioni 123.65 ambapo daraja hilo si tu limebadilisha taswira ya jiji la Dar es Salaam, lakini pia limepunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa magari katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi.
Aidha, Serikali ya Jamhuri ya Koreakupitia benki ya Exim ya Korea pamoja na Shirika la Bima la Korea (Ksure) imeendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza mradi wa reli ya kisasa ya (SGR) ikihusisha utengenezaji wa vichwa na mabehewa ya treni.
‘‘Jumla ya fedha zilizotolewa na benki ya Exim na Ksure kwa ajili ya ununuzi wa vichwa na mabehewa ya treni yanayotengenezwa na Kampuni ya M/S Hyundai Rotem ya Jamhuri ya Korea ni dola za Marekani milioni 302.4”, alieleza Dkt. Mkuya.
Aidha katika mkutano huo, Mhe. Dkt. Mkuya aliiomba Serikali ya Jamhuri ya Korea kuharakisha mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Binguni na mradi wa Uendelezaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutokana na umuhimu wa miradi hiyo katika kutoa huduma za Afya za kibingwa nchini Tanzania.
Akizungumza kuhusu uchumi wa Tanzania Mhe. Dkt. Mkuya alisema kuwa licha ya changamoto ya Covid 19 na vita ya Urusi na Ukraine Uchumi umeanza kuimarika katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2023 ambapo ukuaji uliorekodiwa ulikuwa wa asilimia 5.6 kwa Bara na ulikuwa asilimia 6.2 kwa Zanzibar.
Mhe. Dkt. Mkuya, aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania, kutekeleza ajenda ya Maendeleo ya Taifa kama ilivyoainishwa chini ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 na Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22–2025/26 na Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar 2021 -2026.
Alisisitiza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa ajili ya maendeleo ya watu wetu.
Kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Uchumi na Fedha wa Korea Mhe. Kyungho Choo, alisema kuwa Korea itaendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.