Na. WAF – Songwe
Halmashauri ya Wilaya ya Songwe watapatiwa magari Matatu ya kubebea wagonjwa (Ambulance) ili kusaidia kutoa huduma za dharura na rufaa za matibabu na kupunguza madhara makubwa yanayoweza sababisha vifo kwa wagonjwa wanaohitaji huduma kwa haraka.
Hayo yamesemwa leo Septemba 11, 2023 na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati akiongea na Madaktari, Wauguzi pamoja na timu ya usimamizi wa Afya ngazi ya Halmashauri wakati alipofanya ziara katika Mkoa wa Songwe.
Waziri Ummy amesema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeagiza kila Halmashauri kupata magari ya kubebea wagonjwa Mawili na Wizara ya Afya inatoa gari Moja, jumla Halmashuri hiyo itapata magari matatu.
“Magari haya yatasaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto, lakini pia kurahisisha mgonjwa kupata huduma kwa haraka pale anapopatiwa rufaa au anapohitaji huduma za dharura”. Amesema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amewasisitiza wananchi wa Halmashauri hiyo kujitokeza katika zoezi la utolewaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio linalotarajiwa kuanzia tarehe 21-24 Septemba 2023 ili watoto wao waweze kupata chanjo ya ugonjwa huo.
“Baada ya kupatikana kwa mgonjwa mmoja mwenye ugonjwa wa Polio Mkoani Rukwa Serikali kupitia Wizara ya Afya tumeamua kutoa chanjo hiyo kwa Mikoa Sita ikiwemo Mkoa wa Rukwa, Kagera, Kigoma, Mbeya, Katavi, Songwe hivyo ninawaomba sana wazazi kushiriki kwa kuwatoa watoto”. Amesema Waziri Ummy.
Pia, Waziri Ummy ameiagiza Bohari Kuu ya Dawa Nchini kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba katika Halmashauri hiyo ili Hospitali ya Wilaya ya Songwe ianze kutoa huduma katika sehemu ambazo hazijaanza.
“MSD hakikisheni vifaa tiba vinapatikana kwa wakati na mvigawe katika vituo vya Afya ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Songwe ili huduma zipatikane ikiwemo huduma za uzazi mama na mtoto”. Amesema Waziri Ummy.
Katika ziara hiyo Waziri Ummy ameridhishwa na upatikanaji wa dawa, utolewaji wa huduma pamoja na ujenzi unaoendelea ikiwemo jengo la EMD, Mama na Mtoto, Utawala, Mochwari na jengo la huduma za Mionzi.
“Kwakweli nimeridhishwa na upatikanaji wa Dawa, kwa sasa hatuwezi kumlaumu Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatoa fedha za dawa kwa 100%, Sasa kazi kwetu watendaji tuendelee kuhakikisha Dawa zinapatikana“. Amesema Waziri Ummy.