Wachezaji wa timu ya Kijitonyama Chipukizi wakishangilia baada ya kushinda mashindano ya Healthy Champions (Tanzania Champions Cup) yaliyoshirikisha jumla ya timu 24.
Wachezaji wa timu ya Moshi Academy wakishangilia baada ya kumaliza katika nafasi ya pili ya mashindano ya Healthy Champions (Tanzania Champions Cup) yaliyoshirikisha jumla ya timu 24.
Zoezi la ugawaji wa jezi kwa timu zilizofuzu hatua ya nane bora ya mashindano ya Healthy Champions (Tanzania Champions Cup)
Mratibu wa mashindano Majuto Omary na ma-boss wa Green Sports Africa wakifuatilia mashindano ya Healthy Champions (Tanzania Champions Cup)
Wachezaji wakiwania mpira wakati wa mashindano ya Healthy Champions (Tanzania Champions Cup) yaliyofanyika kwenye uwanja wa Kijitonyama.
Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam.
Timu ya Kijitonyama Chipukizi ya U-21 imetwaa ubingwa wa mashindano ya Healthy Champions (Tanzania Champions Cup) yaliyoshirikisha jumla ya timu 24.
Kijitonyama Chipukizi iliishinda kwa penati 2-0 dhidi ya Moshi ya Buza katika mchezo wa fainali uliofanyika kwenye uwanja wa Kijitonyama.
Mchezo huo ulikuwa mkali na wa kusisimua ambapo kila timu ilikuwa inasaka ushindi kwa ajili ya kupata zawadi nono. Kwa ushindi huo, timu ya Kijitonyama Chipukizi ilishindha kitita cha sh600, 000, kombe na medali za dhahabu wakati Moshi Academy walishinda Sh300, 000 na medali za fedha.
Nafasi ya tatu ilikwenda kwa Madina ambayo iliifunga Young Stars na kuzawadiwa sh200, 000. Akizungumza baada ya mechi ya fainali, kocha wa Kijitonyama Chipukizi, Frank Mnenga maarufu kwa jina la Didi alisema kuwa wamefarijika sana kushinda zwadi hiyo na wachezaji wake wamepata hamasa zaidi.
“Nawapongeza wachezaji kwa kupambana muda wote, haikuwa kazi rahisi na zawadi hii ni kubwa tokea kuanzisha kituo chetu. Fedha hii pia itatusaidia kugharimia gharama mbalimbali katika mashindano ya soka ya Ufukweni ya Shirikisho la Kandanda Tanzania (TFF),” alisema Didi.
Kocha wa Moshi Academy, Mohamed Makange alisema pamoja na kushindwa kutwaa ubingwa, wameyafurahia mashindano kwani ni ya muda mfupi na yenye zawadi nono.
“Fedha tuliyoshinda itatusaidia kununua vifaa vya michezo na chakula kwani wachezaji wetu wanakaa kambini. Tumefurahi sana kushiriki mashindano yenye tija,” alisema.
Mkurugenzi wa Green Sports Africa, George Ouma alisema mashindano hayo yanafanyika kwenye nchi tano ikiwamo Tanzania. “Tanzania ni ya nne nchi nyingine ambazo zimefanya mashindano haya ni Uganda, Ghana na Nigeria. Nchi ya mwisho ni Senegal ambayo yatafanyika mwezi huu pia,” alisema.
Alisema vijana wenye vipaji watakaopatikana kwenye mashindano hayo watapelekwa Marekani na Hispania ambako wataendelezwa vipaji vyao. Mkurugenzi mwenza wa Kampuni ya Green Sports Africa, Kassim Ismaili alishukuru timu zote zilizoshiriki pamoja na mratibu wa Tanzania.