#Awasisitiza mafundi kusikiliza maelekezo ya wataalam wa ujenzi
#Atoa Siku 24 kukamilisha Mradi wa Shule Mpya kwa fedha za SEQUIP Kata ya Namilembe
#Kuzungumza na mafundi na vibarua (wakazi) wa eneo la mradi akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya Elimu na Afya.
Na Dotto Manumbu – Ukerewe
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Ndg. Emmanuel Sherembi amewahakikishia wakazi wa Kata ya Namilembe kuendeleza mageuzi makubwa Sekta ya Elimu na Afya kwa kusimamia vizuri fedha za miradi huku akiendeleza ushirikiano uliopo na wananchi kuleta maendeleo.
Aliyasema hayo Septemba 6, 2023 wakati akiwa katika ziara ya kukagua ujenzi wa miradi ya maendeleo kata za Namilembe na Kagunguli, alisema June 30, 2023 Shule ya Sekondari Busangumugu ilipokea fedha kiasi cha Shilingi Milioni 584 kutoka SEQUIP kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari katika kata ya Namilembe ambapo hadi sasa ujenzi huo unaendelea vizuri.
“Wananchi, tuna kila sababu ya kumshukuru Rais Samia kwa kuelekeza fedha kiasi cha Shilingi Milioni 584 kukamilisha ujenzi wa majengo mawili (2) yenye vyumba vya madarasa yenye thamani ya shilingi Milioni 100, Ujenzi wa majengo mawili yenye vyumba vya madarasa na ofisi moja ya walimu kwa thamani ya shilingi Milioni 109.378, Ujenzi wa jengo moja la utawala lenye thamani ya Shilingi Milioni 77.7, Ujenzi wa jengo moja lenye Maabara ya Kemia na Bailojia kwa thamani ya Shilingi Milioni 102, Ujenzi wa jengo moja lenye Maabara ya Fizikia lenye thamani ya Shilingi Milioni 51, Ujenzi wa Maktaba moja kwa thamani ya Shilingi Milioni 61.9”, alisema.
Sherembi alisema serikali imetoa Shilingi Milioni 51 kwa ajiri ya ujenzi wa chumba kimoja kwa ajiri ya wanafunzi kujifunza masuala ya TEHAMA, Rais Samia amewapatia kiasi cha Shilingi Milioni 10.5 kwa ajiri ya ujenzi wa jengo moja (1) la vyoo vya wanafunzi wavulana ambapo matundu 4 kati yake vitatengenezwa vyoo maalum kwa wanafunzi wenye uhitaji.
“Rais hakuishia hapo, wakazi wa kata hii mmepewa kiasi cha Shilingi Milioni 12.6 kupitia mradi wa SEQUIP kwa ajiri ya ujenzi wa jengo moja la vyoo vya wanafunzi wasichana, matundu manne kati yake yakiwa ni kwa ajiri ya wanafunzi wa kike wenye mahitaji maalum na chumba maalum, Rais ametoa kiasi cha Shilingi Milioni 4.166 kwa ajiri ya ujenzi wa kichomea taka na pia katika shule hii tuliyopo kutafanyika ujenzi wa tanki moja kubwa la maji la ardhini, kiu yetu sisi viongozi na kiu ya Rais wetu Dkt. Samia ni kumwandaa mtoto apate Elimu akiwa katika mazingira rafiki ya ufundishaji na ujifunzaji”, ameongeza.
“Niwahakikishie wakazi, mafundi na vibarua wote tunaoshiriki ujenzi wa shule hii mpya, sisi viongozi wenu, tamaa yetu ni kuhakikisha tunaendeleza mageuzi makubwa kwa kuwaunganisha wananchi na kushiriki kwa pamoja shughuli mbalimbali za maendeleo ili kuikuza Sekta ya Elimu na Afya ambayo itachochea utatuzi wa kero tulizonazo”, alisema Sherembi.
Alisisitiza kuwa mafundi katika miradi yote inayotekelezwa waendelee kuwashirikisha na kuzingatia maelekezo ya wataalam wa Idara ya Ujenzi ili miundombinu hiyo izingatie ubora na viwango vinavyotakiwa na mafundi wahakikishe wanajenga usiku na mchana ili ifikapo Septemba 30 mwaka huu.
Akielezea faida zitakazopatikana baada ya mradi kukamilika Sherembi amesema uwepo wa Shule hiyo katika Kitongoji cha Hamuhama, Kijiji cha Namilembe na katika kata ya Namilembe utasaidia wanafunzi wa vijiji vya Busagami, Bukonyo na Namilembe kusomea ndani ya kata yao tofauti na ilivyo sasa, Shule hiyo itaanza kuwapokea wanafunzi watakaoanza kidato cha kwanza 2024 kukiwa na miundombinu yote.
Nao wananchi na mafundi katika mradi huo akiwepo Jumanne Malobo na Neema Bitwalo wamepongeza jitihada zinazotekelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo hasa upande wa ufuatiliaji wa mwenendo mzima wa ujenzi wa mradi huo na kuahidi kufuata maelekezo ya viongozi wa Idara ya ujenzi.