Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na wananchi waliofika katika kambi maalumu ya siku mbili ya upimaji na matibabu ya moyo inalofanyika JKCI Hospitali ya Dar Group kwaajili ya kupata huduma za matibabu ya moyo.
Mwakilishi wa kampuni ya dawa za binadamu ya Micro Labs Limited – Laborex Tanzania Zawadi Mbasha akizunguma na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge kuhusu dawa za magonjwa ya moyo na kisukari wanazozitoa kwa wananchi waliofika katika kambi maalumu ya siku mbili ya upimaji na matibabu ya moyo inayofanyika JKCI Hospitali ya Dar Group kwaajili ya kupata huduma za matibabu ya moyo.
Mwakilishi wa kampuni ya dawa za binadamu ya Micro Labs Limited – Laborex Tanzania Festus Asenga akimpa dawa ya moyo Selemani Athumani mkazi wa Mbagala aliyefika katika kambi maalumu ya siku mbili ya upimaji na matibabu ya moyo inayofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Fatma Suedy akichukuwa taarifa za wananchi waliofika katika Hospitali hiyo kwaajili ya kupata huduma ya upimaji na matibabu ya moyo wakati wa kambi maalumu ya matibabu ya siku mbili inayofanyika katika Hospitali hiyo.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Christine Yonathan akimpima shinikizo la damu (BP) mpiga picha wa kituo cha Televisheni cha ITV Idrissa Magomeni wakati wa kambi maalumu ya matibabu ya siku mbili inayofanyika katika Hospitali hiyo.
Picha na JKCI
Na Stela Gama – Dar es Salaam
Wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika zoezi la upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo linalofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza na wananchi waliofika katika zoezi la upimaji na matibabu ya moyo linalofanyika katika kambi maalumu ya siku mbili inayofanyika JKCI Hospitali ya Dar Group.
Dkt. Kisenge alisema wananchi wakipata mapema huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo wataisaidia Serikali kupunguza gharama za kulipia matibabu hayo kwani matibabu ya kibingwa ikiwemo upasuaji wa moyo gharama zake ni kubwa.
“Hadi sasa watu 84 wameshapata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo na wengi tuliowaona wanamatatizo ya shinikizo la juu la damu, huu ni ugonjwa ambao tumekuwa tukiwakuta nao wananchi wengi tunaowaona katika maeneo mbalimbali hapa nchini”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema magonjwa ya moyo yamekuwa yakiongoza kwa kuua watu wengi hapa Duniani ambapo kwa takwimu za Shirika la Afya Dunia (WHO) watu milioni 17 wanapoteza maisha kila mwaka kutokana na magonjwa hayo.
“Taasisi yetu imeamua kusogeza upatikanaji wa huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa kuwafuata wananchi mahali walipo, tunahitaji wananchi wenye matatizo ya moyo wapate huduma za matibabu mapema”,.
“Huduma hii inajulikana kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services tunawafuata wananchi mahalli walipo na kutoa huduma za uchunguzi na upimaji wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo na kisukari pia tunatoa ushauri wa jinsi ya kuepukana na magonjwa haya pamoja na elimu ya lishe bora”, alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wao wananchi waliopata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo waliishukuru Serikali kwa huduma waliyoipata na kuomba Taasisi hiyo kutoa huduma hiyo mara kwa mara kwani wengi wao inawawia vigumu kwenda moja kwa moja JKCI kupata matibabu hii ni kutokana na utaratibu uliopo wa kupata rufaa.
“Taratibu za kwenda kutibiwa JKCI kama hauna bima ya afya ni lazima uwe na rufaa na kupata rufaa mlolongo wake ni mrefu, baada ya kuona tangazo hili niliona ni vyema nami nije kufanya uchunguzi wa afya yangu nimepima nakupewa dawa za moyo. Nawaomba wananchi wenzangu tutumie nafasi hii kuja kupima magonjwa ya moyo”, alisema Selemani Athumani mkazi wa Mbagala.
“Niliona tangazo la upimaji huu katika mitandao ya kijamii nikaona nije kupima na kujua kama nina matatizo ya moyo au la hii ni kutokana na maisha ninayoishi sifanyi mazoezi na hata ulaji wangu wa chakula siyo mzuri kwani sili vyakula bora”, alisema Birgitha Boaz mkazi wa River Side.
Naye Festus Asenga mwakilishi wa kampuni ya dawa za binadamu ya Micro Labs Limited – Laborex Tanzania ambao wako katika kambi hiyo kwaajili ya kutoa huduma ya dawa kwa watu wanaokutwa na matatizo ya moyo na kisukari alisema kampuni hiyo iliona waungane na JKCI kwa kutoa dawa bure kwa wananchi watakaokutwa na matatizo.
“Tunatoa dawa za siku 30 bure kwa watu wanaokutwa na matatizo kwani wananchi wengi hawana uwezo wa kununua dawa kwa kufanya hivi tunawasaidia kuanza matibabu mapema”, alisema Asenga.
Katika kambi hiyo ya uchunguzi na matibabu ya moyo ya siku mbili huduma zinazotolewa ni upimaji wa sukari mwilini, urefu, uzito, uwiano baina ya urefu na uzito, shinikizo la damu, elimu ya lishe bora na matumizi sahihi ya dawa, vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi pamoja na umeme wa moyo na dawa za moyo na kisukari