Na.Joctan Agustino,NJOMBE
Simanzi imetawala kwa maelefu ya waombolezaji waliyojitokeza kuaga mwili wa mwanafamilia wa pili kupoteza maisha ndani ya siku mbili ,baada ya majambazi wenye silaha za moto kuvamia nyumbani kwa bwana Golden Luoga(34) na kisha kumpiga risasi yeye na kaka yake ambaye alipoteza maisha saa chache baada ya shambulio hilo August 29 majira ya saa mbili usiku
Katika Tukio hilo ambalo majambazi wawili walivamia nyumbani kwa Golden Luoga na kisha kuwapiga risasi yeye na kaka yake Faraja Luoga(40) aliyefariki dunia saa chache baada ya tukio ,majambazi walifanikiwa kuondoka na begi lenye fedha pamoja na mashine za kufanya miamala ya fedha Kibenki jambo linaloumiza wengi.
Akizungumza wakati wa kuaga mwili wa Golden Luoga aliyefariki dunia Katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya ,Ikiwa ni siku moja tu imepita tangu mwili wa kaka yake uagwe nyumbani hapo aliyefariki saa chache baada ya kupigwa risasi,Msemaji wa familia Edger Mtitu na katibu wa mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini Andrew Mahali wamesema tukio hilo la ajabu limeumiza familia hivyo wanaomba vyombo vya usalama vifanye kilia liwezekanalo kuwatia nguvuni wahusika
“Tunafahamu uwezo wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ni mkubwa hivyo tunaomba nguvu kubwa iongezwe kuwatafuta wahusika wa tukio hili ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao,anasema Edger Mtitu msemaji wa familia”.
Awali akitoa salamu za pole na rambirambi kwa niaba ya wafanyabiashara ,Mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara halmashauri ya mji wa Njombe Eliud Mgeni Pangamawe amesema majambazi wamekatisha uhai wa kijana mdogo aliyekuwa na maono makubwa kwenye biashara na kisha kuomba vyombo vya ulinzi na usalama kuona namna ya kulinda usalama wa wafanyabiashara wa halmashauri ya mji huo kwasababu ya ongezeko la matukio.
Pangamawe amasema kitendo kilichofanyika ni ukatili mkubwa kwasababu kimeondoa maisha ya kijana mdogo msomi ambaye alianza kukua kibiashara .
“Kwa niaba ya wafanyabiashara wa halmashauri ya mji wa Njombe niiombe serikali ,kulingana na hali ya usalama ya sasa ione jinsi gani wafanyabiashara wanaweza kuhakikishiwa usalama ili wafanye biashara bila hofu,Eliud Mgeni Pangamawe Mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara mji halmashauri ya mji wa Njombe “.
Wakati wafanyabiashara na asas mbalimbali zikilaani tukio hilo , Polisi Kupitia kwa kamanda wake mkoa wa Njombe John Imori imesema licha ya kutokea tukio hilo lakini mkoa uko salama hivyo ili kukomesha mikasa hiyo itawasaka wahusika usiku na mchana hadi pale watakapopatikana ili sheria ichukue mkondo wake .
Miili ya marehemu wote wawili inapumzishwa kijiji kwao Ludewa