***********************************
NA EMMANUEL MBATILO
Viongozi wa kisiasa nchini wamezitaka taasisi mbalimbali kuendelea kutoa elimu ya mpiga kura hasa kwa wanawake katika maeneo mbalimbali kuanzia ngazi za chini ili kuwajengea uwezo na kuondoa dhana iliyojengeka ndani ya jamii kuwa wanawake hawawezi.
Wameyasema katika hafla ya uzinduzi wa Taasisi ya Haki yangu Mtanzania ambayo inalenga kutoa elimu kwa wapiga kura Kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na uchaguzi Mkuu.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji Gender Action Tanzania (GATA) Bi.Neema Makando amesema lengo la kuzindua taasisi hiyo ni Kutoa elimu kwa wapiga kura katika kuzingatia taratibu na sheria wakati wa kupiga kura pamoja na uangalizi kwenye madaftari ya kupiga kura.
Aidha Bi.Neema amesema kuwa utoaji elimu huo wataufanya kupitia njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii, vyombo vya habari pamoja na kuzuia udhalilishaji mitandaoni ambapo amewasisitiza wadau mbalimbali kuwaunga mkono ili kufanikisha adhima ya kila mwananchi kupata elimu ya kupiga kura kwa kuifikia mikoa yote 24 hapa nchini.
Kwa upande wake muwasilishaji wa Mada katika hafla hiyo Bw.Rajabu Mzirayi amesema kuwa wanawake wanatakiwa kujengewa misingi mizuri ya kiongozi toka ngazi za chini pamoja na vyanzo vya kujipatia kipato ikiwemo haki ya kumiliki mali za familia ili lengo la kufikia uwiano wa 50 kwa 50 katika uongozi baina yao na wanaume lifanikiwe na kuwa na tija.
Bw.Mzirayi amesema kuwa jitihada za kuelimisha jamii haswa kwenye masuala ya haki za wanawake katika uongozi bado ni changamoto kutokana na wengi wao kushindwa kujiamini, kutokuungwa mkono na wanawake wenzao pamoja na kutokuwepo kwa misingi mizuri ya kisheria ya kuvibana vyama vya siasa na taasisi mbalimbali kutimiza haki za wanawake.
Nae katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Khalifa Suleiman amesema wao kama CUF wamejipanga kuhakikisha wanwapa kipaumble wanawake katika kugombea uongozi kwani mpaka sasa kuna idadi kubwa ya viongozi wa chama wanawake kuliko ilivyozoeleka.