Mkuu wa wilaya ya Mlele Alhaj Majid Mwanga (Kulia) akikabidhi mwenge wa Uhuru kwa mkoa wa Rukwa kwa jiaba ya Mkuu wa mkoa wa Katavi, bi. Mwanamvua Mrindoko.
Viongozi wa dini ni sehemu ya watu waliohudhuria katika makabidhiano hayo ya mwenge wa uhuru
Na. Zillipa Joseph, Katavi
Kiongozi wa Mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2023 Abdalla Shaib Kaim ameupongeza mkoa wa Katavi kwa kumaliza mbio hizo bila ya mradi wowote kukataliwa katika wilaya zake tatu zenye halmashauri tano.
Bwana Kaim amesema mkoa umesimama imara na kufanya kazi kubwa ya kusimamia miradi mbalimbali ambapo amebaini kasi kubwa ya usimamizi wa miradi.
Amesema hayo wakati wa makabidhiano ya mwenge wa uhuru kwa mkoa wa Rukwa.
‘Kwa dhati kabisa niseme mmeutendea haki mwenge wetu wa uhuru, mmeandika historia kubwa, mmetuheshimisha sana hongereni sana wana Katavi. Kwa hakika wanakatavi mmetisha mmeupiga mwingi na chenji imebaki’ alisema Kaim.
Aliongeza kuwa viongozi wa katavi wamemtendea haki Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha fedha za miradi zinatumika kama zilivyopangwa na kwa usahihi kabisa.
‘Tumejionea miradi mizuri ya kimkakati ambayo kwa dhati inatokana na kazi kubwa mnayofanya kiukweli mmefunika’ alisema.
Awali kiongozi mbio za mwenge kitaifa bi. Atupile Mhalila ameipongeza Katavi kwa kutoka na clean sheet katika halmashauri zote tano.
‘Kutoka na clean sheet katika halmasahuri zote si kazi ndogo, hongereni sana’ alisema Atupile.
Pia ameshukuru kwa mapokezi mazuri waliyopata na kuwataka viongozi wote wa katavi kuendeleza mshikamano kwa ajili ya mafanikio zaidi.
Akitoa taarifa kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Katavi, mkuu wa wilaya ya Mlele Alhaj Majid Mwanga amesema mwenge wa uhuru kwa mkoa wa Katavi ulikimbizwa kwa siku tano.
Alhaj Mwanga amesema mbio zimeweza kukimbia kwa kilometa 885 kwa mkoa mzima, kukagua na kutembelea miradi 40, ambapo miradi 22 ilizinduliwa, miradi 8 iliwekwa mawe ya msingi na miradi kumi ilitembelewa.
Jumla ya gharama za miradi yote hiyo ni zaidi ya shilingi bilioni 5.2.
Aliongeza kuwa mkoa wa Katavi umetekeleza kauli mbiu ya mbio za mwenge wa uhuru kwa kuhifadhi mazingira ambapo wameandaa miche ya miti zaidi ya milioni saba ambayo imepandwa sehemu mbalimbali zikiwemo taasisi na katika vyanzo vya maji.