Tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 300,000 za maji linalojengwa katika mradi wa maji Matiri Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbinga Mhandisi Mashaka Sinkala aliyeshika fimbo,akimuonyesha Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa wakala wa usambazaji maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)Mhandisi Lucy Koya katikati, mchoro wa mradi wa maji Matiri utakaohudumia zaidi ya wakazi 9,870 wa kijiji cha Matiri na Kihaya, wa kwanza kulia Kaimu Mkurugenzi wa Ruwasa Bwai Biseko.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa wakala wa usambazaji maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)Mhandisi Lucy Koya akipanda ngazi kukagua ubora wa tenki la kuhifadhi maji la lita 300,000 linalojengwa katika mradi wa maji Matiri wilayani Mbinga.
Kaimu Mkurugenzi wakala wa usambazaji maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)Bwai Biseko akipanda ngazi kukagua ujenzi wa tenki la maji katika kijiji cha Matiri wilayani Mbinga wakati wa ziara ya wajumbe wa Bodi ya Ruwasa kutembelea miradi ya maji wilayani humo,anayemuangalia chini meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbinga Mashaka Sinkala.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa wakala wa usambazaji maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)Mhandisi Lucy Koya katikati,akimsikiliza meneja wa Ruwasa mkoa wa Ruvuma Mhandisi Rebman Ganshonga kushoto kuhusu maendeleo ya ujenzi wa mradi wa maji Matiri utakaohudumia vijiji viwili vya Matiri na Kiyaha Halmashauri ya wilaya Mbinga,kulia meneja wa Ruwasa wilayani humo Mhandisi Mashaka Sinkala.
Na Muhidin Amri,
Mbinga
WAKALA wa usambazaji maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wilayani Mbinga,imeanza kutekeleza mradi wa maji wa Matiri ili kupunguza adha ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi 9,870 wa vijiji vya Matiri na Kiyaha.
Aidha mradi huo,utasaidia kupungua kwa magonjwa ya mlipuko na kuwezesha wananchi kupata muda mwingi wa kufanya shughuli nyingine za kiuchumi kwa kuwa maji yatapatikana kwenye makazi yao.
Hayo yamesemwa jana na meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbinga Mashaka Sinkala,wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo kwa wajumbe wa bodi ya Wakurugenzi wa Ruwasa walioko kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji mkoani Ruvuma.
Sinkala alisema,mradi wa maji Matiri ulianza kutekelezwa Mwezi Mei kupitia Mkandarasi kampuni ya M/S Sivikwa Co.Ltd kwa gharama ya Sh.milioni 726,360,390.00 na unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba 2023.
Alisema, muda wa utekelezaji wa mradi ni miezi sita na hadi sasa umefikia asilimia 60 na hakuna fedha iliyolipwa kwa mkandarasi na Ruwasa imehusika kwa kununua mabomba kwa gharama ya Sh.milioni 724,660,270.00 hivyo kufanya gharama halisi kuwa Sh.bilioni 1,451,020,660.00.
Sinkala ametaja kazi zilizopangwa kufanyika ni ujenzi wa tenki la lita 300,000,kuchimba mitaro na kulaza mabomba umbali wa kilomita 26,669 ujenzi wa vituo 17 vya kuchotea maji,ujenzi wa chanzo,ununuzi wa dira za maji 317 na kujenga ofisi ya Jumuiya ya watumiaji maji(CBWSO).
Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya Ruwasa Lucy Koya,amefurhishwa na Mkandarasi kampuni ya Sivikwa Co. Ltd kwa uwezo,uzalendo na uadilifu mkubwa katika kutekeleza mradi huo.
Pia alisema,kampuni hiyo imeonyesha uzalendo mkubwa kwa serikali ya awamu ya sita kwa kuanza kutekeleza mradi huo unaolenga kumaliza kero ya huduma ya maji kwa wananchi bila kupewa fedha na serikali.
“kama mwenyekiti wa Bodi ya Ruwasa nimefarijika sana na kazi ya mkandarasi huyu,ametekeleza mradi kwa asilimia 60 bila kupata advance,naiomba menejimenti ya Ruwasa endeleeni kumpa ushirikiano kwa kumpatia kazi nyingine”alisema Mhandisi Koya.
Ameuagiza uongozi wa Ruwasa makao makuu,kuhakikisha inaharakisha mchakato wa malipo ya fedha zilizoidhinishwa kutumika katika mradi huo ili mkandarasi aweze kukamilisha kazi haraka na wananchi wapate huduma ya maji kwenye maeneo yao.
Kaimu mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Bwai Biseko alisema,moja ya malengo ya kuanzishwa kwa mradi huo ni kusaidia kutoa ajira kwa wananchi wa maeneo husika ili waanze kunufaika na uwekezaji unaofanywa na Serikali yao kupitia miradi ya maji.
Biseko,amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya maji wilayani humo kutekeleza makubaliano yaliyopo kwenye mikataba na watendaji wa Ruwasa ngazi ya wilaya na mkoa kuhakikisha wanasimamia mikataba hiyo.
Msimamizi wa mradi kutoka kampuni ya Sivikwa Co.Ltd Stanley Mlelwa alisema,hadi sasa kazi zilizofanyika ni ujenzi wa tenki kwa asilimia 65,ujenzi wa chanzo,ulazaji wa bomba ambapo maji yameshafika kwenye eneo la tenki.
Alisema,wamejipanga kukamilisha mradi huo kwa muda uliopangwa licha ya changamoto hasa katika uchimbaji wa mitaro ya kulaza mabomba kutokana na jiografia ya mji wa Matiri ambayo sehemu kubwa ni milima mabonde.