Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Hamid Seif Said akizungumza na,Wazazi na Wasanii wa mashairi kuhusiana na thamani ya Walimu wa Madrasa wakati wa Bonaza la mashairi ya papo kwa papo lililofanyika Viwanja vya Skuli ya Kiwengwa Kumbaurembo.
Wanafunzi wa Madrasa za Kiwengwa Kumbaurembo wakifuatilia Bonaza la mashairi ya papo kwa papo lililofanyika Viwanja vya Skuli ya Kiwengwa Kumbaurembo.
Wanafunzi wa Skuli ya Makunduchi wakitoa burudani ya Ushairi wenye maudhui ya kutambua thamani ya Mwalimu wa Madrasa wakati wa Bonaza la Mashairi ya Papo kwa papo lilifanyika Viwanja vya Skuli ya Kiwengwa Kumbaurembo.
Wasanii wa Mashairi kutoka Chama cha Kuwaendeleza Washairi Zanzibar CHAKUWAZA wakisoma utenzi wenye maudhui ya kutambua thamani ya Mwalimu wa Madrasa wakati wa Bonaza la Mashairio ya Papo kwa papo lilifanyika Viwanja vya Skuli ya Kiwengwa Kumbaurembo.
Vijana wa Sarakasi Mkoa wa Kaskazini Unguja wakionyesha Mchezo huo wakati wa Bonaza la mashairi ya papo kwa papo lililofanyika Viwanja vya Skuli ya Kiwengwa Kumbaurembo.
Wasanii wa Mashairi Kassim Yussuf (zero kasorobo) na Issa Ali (Daktari wa mashairi) wakitoa burudani ya Ushairi wenye maudhui ya kutambua thamani ya Mwalimu wa Madrasa wakati wa Bonaza la Mashairi ya Papo kwa papo lilifanyika Viwanja vya Skuli ya Kiwengwa Kumbaurembo.
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Hamid Seif Said akikabidhi misahafu kwa Walimu wa Madrasa za Kiwengwa Kumbaurembo wakati wa Bonaza la mashairi ya papo kwa papo yalilenga kuelimisha jamii juu ya thamani ya walimu wa Madrasa huko Viwanja vya Skuli ya Kiwengwa Kumbaurembo.
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Hamid Seif Said akisikiliza maelezo kutoka kwa msanii wa Mashairi Kassim Yussuf (zero kasorobo) wakati alipofika Viwanja vya Skuli ya Kiwengwa Kumbaurembo kushiriki Bonaza la Mashairi ya Papo kwa papo.
PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO ZANZIBAR
Na Rahma Khamis Maelezo
Mkuu wa Wilaya ya kaskazini “B” Hamid Seif Said ameitaka jamii kutambua na kuthamini mchango unaotolewa na walimu wa Madrasa katika kuwapatia maelezi bora watoto wao.
Akizungumza na wazazi ,walimu na wanafunzi wa Madrasa za Shehia ya Kiwengwa Kumbaurembo katika Bonaza la mashairi ya papo kwa papo amesema walimu hao wamekuwa na kazi ngumu yakujitolea.
Amesema waalimu wa Madrasa wanajitahidi katika kuwafundisha watoto malezi mema kwani muda mwingi watoto hao wanakuwepo chini ya uangalizi wao hivyo ni vyema kuthamini mchango wanaoutoa bila ya malipo.
“Waalimu wanatumia nguvu nyingi kusimamia vizuri malezi ya watoto wetu, kwani tunapowawezesha na kuthamini michango yao wataongeza ari na kasi ya kufundisha na kuwafanya kuwa watoto wema na bora katika jamii”alisema Mkuu wa Wilaya.
Aidha amesema kuwa wazazi wamekuwa wakitumia gharama kubwa kuwapeleka watoto Skuli na kusahau thamani na mchango wa waalimu wa Madrasa kwa watoto wao jambo ambalo linarejesha nyuma maenedleeo ya walimu hao .
Ameongeza kuwa waalimu wanatumia muda mwingi kubaki na watoto Madrasa jambo linalopelekea kukosa nafasi ya kujitafutia baadhi ya mahitaji ya lazima hivyo ipo haja ya kuwawezesha walimu hao kuweza kujikimu katika mahitaji yao.
“ Ongezeko la madawa ya kulevya na Udhalilishaji linachangiwa na ukosefu wa malezi bora ya watoto wetu ,ambao unachangiwa na kutokuwathamini walimu wa madrasa hivyo tushirikiane na walimu hao katika malezi ili kuondoa changamoto hizo ” ,alisema.
Aidha Mkuu huyo aliwasisitiza wazazi kukaa na watoto wao kiurafiki zaidi ili kuwapa fursa ya kutoa taarifa za udhalilishaji pindi wanapo kumbana nazo.
Akizungumzia suala la wasanii amefahamisha kuwa watunzi wa mashairi ni wasanii kama wasanii wengine kwani wanaelimisha jamii juu ya mambo mbali mbali ikiwemo athari za matumizi ya madawa ya kulevya,maradhi yasioambukiza na malezi ya watoto.
Akitoa maelezo mafupi kuhusu Bonanza la Mashairi hilo Katibu wa Chama cha Kuendeleza Washairi (CHAKUWAZA) Maimuna Hashim
amesema lengo la Bonaza hilo ni kuihamasisha jamii kuatambua thamani ya walimu wa madrasa,pamoja na kutoa elimu juu ya athari za matumizi ya dawa za kulevya na maradhi yasioambukiza kupitia Sanaa za mashairi.
Katibu ameeleza kuwa chama cha kuendeleza washairi kinafanya kazi kwa kujitolea na kimefanikiwa kutoa elimu kwa jamii,kupitia mashairi, kukuza lugha ya Kiswahili na kuendeleza utamaduni.
Alifahamisha kuwa Bonanza Hilo ni la Tatu Kufanyika kwa mwaka huu ambapo Bonaza la kwanza lilifanyika Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja likiwa na lengo la kuhamasisha jamii juu ya kupinga vitendo vya udhalulishaji.
Aidha ameiomba jamii kufika chama cha washairi kupata washairi waliosajiliwa kuweza kutumia sanaa zao katika shughuli mbalimbali wanazozifanya.
Nao wazazi na walezi wa watoto hao wameahidi kuongeza umoja na ushirikiano kwa waalimu wa Madrasa ili kuzidisha malezi bora ya watoto wao kwani kufanikiwa katika malezi kutasaidia kuondoa vitendo vya udhalilishaji.
Jumla ya shilingi laki tano za Kitanzania zilipatikana kwa ajili ya walimu wa Madrsa za Kiwengwa Kumbaurembo katika Harambee iliyofanyika kwenye Bonaza hilo .