Upimaji wa barabara hiyo ya kiwango cha lami yenye urefu wa mita 745 ukiendelea.
Barabara ya lami iliyopo Kijiji cha Isinde, halmashauri ya Nsimbo
Na Zillipa Joseph, Katavi.
Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 umeweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami yenye urefu wa mita 745, wenye thamani ya shilingi 491, 583,240.63 katika kijiji cha Isinde kata ya Mtapenda halmashauri ya Nsimbo Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi uliolenga kuhudumia jamii.
Halmashauri ya Nsimbo ina mtandao wa barabara wenye jumla ya urefu wa kilomita 511.18 ; kati ya hizo ni kilomita 2.14 tu ndio barabara za lami, huku kilomita 111.308 ni za changarawe na kilomita 397.622 ni barabara za udongo.
Akiweka jiwe la msingi katika.mradi huo Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2023.Abdallah Shaib Kaim amesema serikali kwa kutambua umuhimu wa miundombinu ya barabara nchini imekuwa ikitoa fedha nyingi za kujenga barabara zitakazochochea ukuaji wa maendeleo ya wananchi wake.
Katika hatua nyingine kiongozi huyo wa mbio za Mwenge kitaifa ametoa siku tano kwa uongozi wa halmashauri hiyo kufanya marekebisho ya barabara hiyo ya Mita 745 baada ya mwenge wa uhuru kubaini kuna mapungufu kadhaa.
‘Na kwa kutambua mkandarasi bado yupo site aitwe aelekezwe na sehemu hiyo ifanyiwe marekebisho na baada ya kufanya marekebisho tunahitaji taarifa ya utekelezaj wa marekebisho pamoja na picha za kabla na baada na video wakati mkandarasi akiwa anafanya marekebisho’ Alisema Kaim.
Aidha amemwomba Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Jamila Yusuf kushirikiana kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kuona marekebisho’ hayo yanafanyika kwa wakati.
Awali Meneja wa TARURA Wilaya ya Mpanda, Mhandisi Hoza Joseph akisoma taarifa ya mradi huo amesema kuwa mradi wa barabara ya Isinde uliibuliwa na Wakala wa barabara Vijijini na Mjini (TARURA) mwaka wa fedha 2022/23,ukiwa na lengo la uboreshaji na uimarishaji wa barabara katika mji wa Nsimbo.
Mhadisi Joseph amesema ujenzi wa barabara ya lami ulianza kutelekezwa Septemba, 2022 na kukamilika Februari 2023 kwa hatua ya ujenzi wa lami nyepesi na mifereji ya mawe ambapo kazi zilizobaki ni uwekaji wa alama za barabarani na usimikaji wa taa ambapo gharama ya ujenzi wa lami ni zaidi ya fedha Mil 491.
Mbunge wa Jimbo la Nsimbo Mkoa wa Katavi, Anna Lupembe amesema kuwa serikali inafanya kazi kubwa ya kuhakikisha miradi mbalimbali ya maendeleo inajengwa katika Jimbo la Nsimbo kama sehemu ya kuwahudumia wananchi.
Lupembe ameipongeza serikali kwa kuimarisha miundombinu ya barabara ambapo kwa sasa mtandao wa barabara za lami unaendelea kuongezeka.
Aidha katika halmashauri ya Nsimbo umekimbizwa Km 198 na kupitia jumla ya miradi 10 yenye thamani ya Fedha zaidi ya milioni 897.