Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,,Kazi,Vijana,Ajira na Wenye ulemavu Profesa Joyce Ndalichako akimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Neema Maghembe kwa kusimamia vema mradi wa ujenzi wa chuo cha Ufundi stadi na marekebisho kwa ajili ya watu wenye ulemavu katika kijiji cha Liganga Songea
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,,Kazi,Vijana,Ajira na Wenye ulemavu Profesa Joyce Ndalichako akikagua mradi wa ujenzi wa chuo cha Ufundi stadi na marekebisho kwa ajili ya watu wenye ulemavu katika kijiji cha Liganga Songea,mradi huo hadi kukamilika unatarajia kutumia shilingi bilioni moja
Na Albano Midelo,Songea
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na Wenye ulemavu Profesa Joyce Ndalichako amekagua mradi wa watu wenye ulemavu katika Kijiji cha Liganga wilayani Songea mkoani Ruvuma unaotarajia kugharimu shilingi bilioni moja hadi kukamilika.
Profesa Ndalichako amekagua mradi huo wa Chuo cha Ufundi Stadi na marekebisho kwa watu wenye ulemavu unaotekelezwa kwa njia ya force account ambao unatarajia kukamilika Oktoba 30 mwaka huu.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo kwa Waziri Ndalichako,Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Songea Neema Maghembe amesema mradi huo unatekelezwa katika awamu mbili ambapo katika awamu ya kwanza inajengwa miundombinu ya vyumba kumi vya madarasa na bweni lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 40.
Maghembe ameongeza kuwa katika awamu hiyo pia inajengwa nyumba moja yenye uwezo wa kuchukua familia tatu ambapo amesema wanatarajia kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Amezitaja changamoto zilizopo kwenye mradi huo kuwa ni ukosefu wa maji ya kutosha kutokana na chanzo cha maji kuwa mbali na eneo la mradi,kuongezeka kwa gharama za vifaa na gharama ya usafirishaji kutoka mjini Songea.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo Waziri Prof.Ndalichako amepongeza usimamizi mzuri wa mradi huo hali ambayo amesema imesababisha kuwa na ubora wa majengo yanayoendana na thamani ya fedha.
“Nimekagua majengo ya mradi huu nimegundua mradi unatekelezwa katika viwango na ubora wa juu,naamini mradi utakamilika ndani ya muda uliopangwa’’,alisisitiza Prof.Ndalichako.
Waziri Ndalichako ameahidi kushughulikia changamoto zote zilizojitokeza ili kuhakikisha mradi huo unakamilika na kuanza kuwahudumia watu wenye ulemavu.
Amelitaja lengo la Rais Dkt.Samia kutoa fedha za kujenga chuo hicho ni kutoa fursa ya ufundi stadi kwa watu wenye ulemavu na kufanya marekebisho ili kuwapunguzia makali ya ulemavu ili waweze kuchangia maendeleo ya Taifa.
Waziri Profesa Ndalichako amefanya ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Ruvuma kwa kutembelea wilaya ya Songea.