Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma Hamza Mwenda akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo katika kipindi cha miezi mitatu kuanza Machi hadi Juni 2023 kwenye mkutano na wanahabari ndani ya ukumbi wa TAKUKURU Mahenge mjini Songea,kulia kwake ni Afisa wa TAKUKURU Ruvuma
Na Albano Midelo,Songea
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoani Ruvuma imebaini mapungufu kwenye miradi mitano ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3.7.
Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo kwa wanahabari katika kipindi cha kuanzia Machi hadi Juni,2023,kwenye ukumbi wa TAKUKURU Mahenge mjini Songea,Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma Hamza Mwenda amesema hatua mbalimbali zimechukuliwa ili kuondoa mapungufu kwenye uchunguzi huo.
“Tumefuatilia utekelezaji wa miradi kumi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 4.9,katika ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi hiyo miradi mitano yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3.7 ilikutwa na mapungufu nah atua zilichukuliwa kuondoa mapungufu hayo’’,alisema.
Mkuu wa TAKUKURU ameitaja miradi yenye mapungufu kuwa ni mradi wa maji katika vijiji vya Masuguru na Mchoteka wilayani Tunduru unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 2.4 ambapo ameitaja changamoto iliyobainika kuwa ni ucheleweshaji upatikanaji vifaa ambapo RUWASA imeshauriwa kutafuta malighafi mapema.
Miradi mingine ameitaja kuwa ni ujenzi wa bwalo la chakula katika shule ya sekondari Limbo wilayani Nyasa unaogharimu shilingi milioni 150 na kwamba mradi upo nyuma ya wakati ambapo Kamati ya Usimamizi wa mradi ilishauriwa kufanya kazi kwa haraka ili kukamilisha mradi huo.
Mkuu wa TAKUKURU ameitaja miradi mingine iliyochelewa kukamilika kuwa ni mradi wa matengenezo ya muda ya barabara za Liula-Mhongozi yenye urefu wa kilometa 13.99, barabara ya Matiri,Kindimba juu hadi Mkongotingisa yenye urefu wa kilometa 26.3,barabara ya Ngeruka hadi Matiri yenye urefu wa kilometa 25.16,ujenzi wa daraja la Mto Kaudongo na ukarabati wa daraja la Mto Mnywamaji ambapo miradi yote imegharimu zaidi ya shilingi milioni 374.
Ameitaja miradi mingine yenye mapungufu inayosimamiwa na TARURA kuwa ni matengenezo ya barabara za Manispaa ya Songea ambazo zimetengewa zaidi ya shilingi milioni 250 na matengenezo ya barabara za wilaya ya Namtumbo ambazo zilitengewa zaidi ya shilingi milioni 567.
Hata hivyo Hamza amebainisha kuwa katika kipindi hicho TAKUKURU kupitia uelimishaji wa umma imeweza kuimarisha klabu za wapinga rushwa 61 za shule za msingi na sekondari,kuendesha mikutano ya hadhara 21,vipindi nane za redio,maonesho kumi na kuandaa Makala za uelimishaji tisa.
Amesisitiza kuwa kupitia uelimishaji umma idadi ya wananchi wanaokwenda TAKUKURU kupata ufafanuzi wa changamoto mbalimbali imeongezeka.