********************************
Na Silvia Mchuruza.
Bukoba,
TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa Mkoa wa Kagera Jana ( Leo ) imemfikisha mahakamani kaimu Meneja Mkuu wa kampuni ya Ranchi za Taifa ( NARCO ) kwa kuomba rushwa ya shilingi milioni 12.
Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera,Bw.John Joseph, alisema kaimu meneja Mkuu wa kampuni ya Ranchi za Taifa ( NARCO )Prof.Philemon Wambura amefikishwa mahakama ya hakimu mkazi Bukoba kwa tuhuma za rushwa.
Bw.Joseph,alisema Prof.Wambura anakabiliwa na tuhuma za rushwa ikiwa ni pamoja na kuomba na kupokea rushwa ,matumizi mabaya ya ofisi,ubadhilifu na uhujumu uchumi kinyume na sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa sheria namba 11 ya mwaka 2007.
Alisema taasisi hiyo ikiwa katika utekelezaji wa majukumu yake ya kuzuia na kupambana na rushwa Septemba 23 mwaka huu ilipata taarifa kutoka vyanzo vyake ambavyo vilionyesha kuwa Prof.Wambura kaimu meneja Mkuu NARCO,amekuwa akijihusisha na vitendo dhidi ya rushwa ikiwemo kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa baadhi ya wafugaji wenye uhitaji wa Vitalu vya kufugia Ng’ombe wenye vitalu ambao wanahitaji kuhuisha mikataba yao ya awali.
Alisema taarifa ya uchunguzi imeonyesha kuwa January 3, 2018 Prof.Wambura Prof.Wambura akiwa kaimu meneja Mkuu wa NARCO alipokea kiasi cha shilingi milioni 12 kutoka kwa mtu mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa ili aweze kumpatia kitalu kwaajili ya kufanyia shughuli za ufugaji huku akifahamu kuwa jambo hilo ni kosa na kinyume cha sheria.
Wakati huohuo alisema kuwa taasisi hiyo imewafikisha watu wengine wanne kwa makosa mbalimbali Octoba 25 mwaka huu.
Amewataka watu hao kuwa ni Stanslous Katto mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa shule ya sekondari Kashenye kwa makosa ya kugushi ,kujipatia mamlaka asiyokuwanayo na kuwasilisha nyaraka zenye maelezo ya uongo kwa mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Missenyi kwa lengo la kujipatia kiasi cha shilingi milioni 5.7.
Alisema uchungunzi ulibaini kuwa Juni 09,2015 Katto,alighushi alighushi sahihi ya mwenyekiti wa serikali ya Kijiji cha Bukwali jina linahifadhiwa na kughushi sahihi ya mkandarasi pia jina linahifadhiwa na jina la kampuni.
Aliwataja wengine kuwa ni Richard Kavogoro mwenyekiti wa Kijiji cha Mkalinzi ,Josephat Nzeye mtendaji wa Kijiji cha Mkalinzi na Onesmo Tiara ambaye alikuwa mwenyekiti wa Vocha za pembejeo wa Kata Muganza halmashauri ya Ngara.
Alisema wote wamefikishwa katika mahakama ya wilaya Ngara kujibu tuhuma zinazowakabili za kutumia nyaraka kwa lengo la kumdangaya mwajiri.
Alisema taarifa ya uchunguzi imeonyesha kuwa zoezi la ugawaji wa Vocha za pembejeo kwa wakulima msimu wa wa 2016/2017 kwa nyakati tofauti katika Kijiji cha Mkalinzi Kata ya Muganza kulifanyika udanganyifu.
Alisema baadhi ya majina ya wanufaika sahihi zao zilighushwa ili kuonyesha kuwa wamepokea mbolea ya ruzuku wakati si kweli.