Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Askari Polisi Wilaya ya Bagamoyo wametakiwa Kubadilika kifikra na kufanya kazi kwa weledi na kuachana na utendaji kazi wa mazoea.
Hayo yalisemwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Pius Lutumo wakati wa ziara yake ya Ukaguzi wa kuangalia utendaji wa kazi Wilayani hapo wakati akizungumza na Maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali ambapo amewataka kuzingatia ufanyaji kazi kwa mujibu wa Sheria za nchi na kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kupeleka utendaji usioridhisha.
Pia, Kamanda Lutumo alisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa nidhamu na kuzingatia maadili ya Jeshi la Polisi kwa kujiepusha na vitendo vya mmomonyoko wa maadili vitakavyolichafua Jeshi ambavyo huweza kusababisha kufukuzwa kazi.
Kadhalika, aliwataka askari kufanya kazi kwa kusimamia misingi ya utendaji bora kwa kutenda haki kwa tunao wahudumia vituoni .
” Wananchi hawapendi kuja kwenye vituo vyetu ila wanafika kwa kuwa wanashida zinazohitaji kusaidiwa nasi hivyo ni jukumu letu kuwapa huduma bora wanapofika kwenye vituo vyetu vya Polisi”,
Aidha, aliwakumbusha askari umuhimu wa kutunza vizuri vielelezo na kutokuwa na tamaa au kushawishika katika kuiba vielelezo hivyo viwapo kituoni.
“Ni jukumu letu kulinda vielelezo vilivyopo kituoni na kuhakikisha vinatunzwa vizuri na siyo kuwa sehemu ya upotevu wa vielelezo hivyo ambavyo vitatumika kama ushahidi Mahakamani.