Na Mwamvua Mwinyi …
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Chalinze, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Sophia Lyidenge amewataka wafanyakazi wa mradi wa umeme wa Serikali kuwa na nidhamu na kutokujihusisha na vitendo vya kihalifu.
Amebainisha hayo, wakati alipotembelea mradi huo wakati akizungumza na wafanyakazi hao kuona kama wana changamoto zozote za kiusalama.
SSP Lyidenge aliwaeleza wafanyakazi hao kuwa wameaminiwa na Serikali kufanya kazi hivyo wanatakiwa kuwa waadilifu na wasijihusishe na vitendo vya kihalifu ikiwemo wizi wa vitendea kazi .
Aliwataka wawe walinzi wa kwanza wa vifaa hivyo.
Sambamba na hayo SSP Lyidenge aliwasihi viongozi wa mradi huo kuwa na mahusiano mazuri na wafanyakazi ikiwemo lugha nzuri yenye staha ili kuongeza hamasa ya utendaji na kufikia malengo ya mradi kwa wakati uliokusudiwa.
” Niwaombe viongozi kuwatia moyo na kuwa na lugha shawishi kwa mnao wasimamia ili mradi huu uweze kukamilika kwa wakati, lugha zisizo na staha huwavunja moyo watendaji na kujikuta ikiwapunguzia morali ya kujituma”.
Sote tunatambua umuhimu wa mradi huu utakavyochochea maendeleo ya kiuchumi kwa kwa wakazi wa Chalinze, Mkoa wa Pwani na taifa kwa ujumla” alisema Lyidenge