Kaimu Meneja wa Uwanja wa Benjamin Mkapa Bw. Milinde Mahona akichangi katika moja ya vipindi akiwa darasani wakati wa mafunzo wakiwa katika Chuo cha Kiataifa Hunnan kilichopo Jimbo la Hunnan katika jiji la Changsha nchini China.
Baadhi ya watumishi kutoka katika mataifa ya Tanzania, Djibouti, Kambodia na Palestina wakiwa katika picha ya pamoja na wataalam wabobezi katika uendelezaji, usimamizi na uendeshaji wa miundombinu ya michezo katika Chuo cha Kiataifa Hunnan kilichopo Jimbo la Hunnan katika jiji la Changsha nchini China.
Na Eleuteri Mangi, WUSM, Dar es Salaam
Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo inaboresha utendaji kazi wa michezo ambapo imewapeleka wataalamu wa miundombini nchini China kupigwa msasa juu ya namna bora ya kuendesha michezo na usimamizi wa miundombinu ya michezo nchini.
Katibu Mkuu wizara hiyo Bw. Saidi Yakubu amesema wataalam wanaohudhuria mafunzo hayo katika Chuo cha Kimataifa Hunnan kilichopo Jimbo la Hunnan katika jiji la Changsha nchini China ni Kaimu Mkuriugenzi wa Maendeleo ya Michezo Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Eliofoo Nyambi, Kaimu Meneja wa Uwanja wa Benjamin Mkapa Bw. Milinde Mahona na Meneja wa Uwanja wa Uhuru Bi. Redemta Nyaonge.
“Tumewapeleka wataalam wetu hawa kujifunza namna bora ya kuendesha viwanja vyetu vya michezo kitaalam, namna ya kusimamia uwanja na vifaa vya michezo na yakushughulikia majanga yanapotokea kulingana na viwango vya CAF na FIFA” amesema Katibu Mkuu Bw. Yakubu.
Lengo la mafunzo hayo ambayo yameanza Agosti 1 hadi 21, 2023 ni kuwajengea uwezo na kuwaongezea ujuzi katika kuendeleza miundombinu ya michezo ikiwemo ujenzi na usimamizi wenye ufanisi wa kisasa na kudumu.
Mafunzo hayo yanashirikisha pia washiriki 19 kutoka katika mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania, Djibouti, Kambodia na Palestina yakifundishwa na wataalam wabobezi katika uendelezaji, usimamizi na uendeshaji wa miundombinu ya michezo kwenye kuzingatia misingi, mahitaji na ufanisi ili kutimiza kwa uhakika lengo la kuwepo kwayo.
Aidha, mafunzo hayo ya nadharia yanaenda sambamba na ya kutembelea viwanja na miundombinu mikubwa ya michezo nchini China kujifunza uendeshaji kwa vitendo na kushuhudia mashindano mbalimbali pamoja na kutembelea viwanda vya vifaa vya michezo na vya ujenzi wa viwanja.
Akiongea kwa njia ya simu kutokea China, Kaimu Meneja wa Uwanja wa Benjamin Mkapa Bw. Milinde Mahona amesema mafunzo hayo yanatija na yatawasaidia kutekeleza majukumu yao ili watanzania wapate burudani kupitia michezo kulingana na sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayotolewa na vyama na mashirikisho ya michezo nchini, Afrika na duniani.