Kaimu Meneja wa RUWASA Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi Joanes Martine akisoma taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha robo ya nne ya mwezi Aprili hadi Juni mwaka 2023 kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kilichofanyika Mji mdogo wa Orkesumet.
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MBUNGE wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo wamewapongeza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa namna wanavyotoa huduma ya maji kwa jamii.
Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani, Ole Sendeka amesema RUWASA Wilaya ya Simanjiro ni miongoni mwa taasisi za Serikali zinazotekeleza ipasavyo wajibu wao.
Amesema RUWASA kupitia viongozi wake Kaimu Meneja wa Wilaya ya Simanjiro, mhandisi Joanes Martine na Meneja wa mkoa huo mhandisi Walter Kirita, wanastahili pongezi kutokana na utendaji kazi wao.
“Nawapongeza mno RUWASA ndiyo sababu hata Bungeni niliwapongeza mhandisi Martine na bosi wake mhandisi Kirita kwa namna wanavyotatua tatizo la maji kwa jamii,” amesema Ole Sendeka.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga amesema RUWASA wanastahili pongezi nyingi kwa namna wanavyotekeleza miradi hivyo taasisi nyingine ziwaige.
Diwani wa kata ya Ngorika, Albert Msole amesema mhandisi Martine anafanya kazi nzuri kwenye eneo hilo kupitia vyombo vya utoaji huduma ya maji ngazi ya jamii (CBWSO’s).
Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Simanjiro, mhandisi Joanes Martine amesema wanatoa huduma kwenye kata 12 zenye vijiji 45 sawa na asilimia 72.6 ya wakazi wa wilaya hiyo.
Mhandisi Mane amesema kata za Mirerani, Shambarai na Endiamtu, zinahudumiwa na mamlaka ya maji Arusha na kata za Orkesumet, Edonyongijape na Langai, zinahudumiwa na mamlaka ya maji Orkesumet.
Amesema hadi kufikia Juni mwaka 2023 hali ya upatikanaji wa maji Simanjiro ni asilimia 58.6 ya wakazi wote kupitia vyanzo vya visima virefu 76, visima vifupi 15, mabwawa madogo 28, wabwawa makubwa 15, chemchem 12 na mto Ruvu.
“Tumeendelea kupata ushirikiano wa viongozi wa wilaya, kata na vijiji, vyenye utekelezaji wa miradi na jamii kutoa maeneo yao kwa hiyari bila fidia ambapo miundombinu na maji imejengwa,” amesema mhandisi Martine.
Amesema wanaendelea kufanya matengenezo ya mara kwa mara katika maeneo yote pindi inapohitajika na kuendelea kuhamasisha jamii kutunza vyanzo vya maji na mazingira.
Amesema wana changamoto ya upungufu wa maji kwenye vyanzo kwa ajili ya matumizi ya mifugo na binadamu na kuharibika kwa jenereta na mota za kusukuma maji, mara kwa mara.