MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Mohamed Ali Kawaida, akiwahutubia Wanachama wa CCM na Wananchi kwa ujumla wa Mkoa wa Kaskazini Unguja katika uwanja wa Chaani.
NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR.
MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Mohamed Ali Kawaida, amevionya baadhi ya Vyama vya upinzani kuacha siasa za chokochoko zinazolenga kukwamisha juhudi za maendeleo nchini.
Hayo ameyasema katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Chaani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kupitia mkutano huo alisema UVCCM iataendelea kulinda,kutetea na kusimamia maslahi ya Serikali zinazotoka na Chama Cha Mapinduzi.
Katika maelezo yake Mwenyekiti Kawaida, alivikumbusha vyama hivyo vya upinzani kuwa kizazi kilichofanya Mapinduzi 1964 bado kipo hai, na sasa kimejielekeza katika utetezi wa Chama,Serikali na viongozi wake.
“Nasaha zangu kwa upinzania wasitumie vibaya fursa ya mikutano ya hadhara kama kichaka cha kutekeleza mipango yao miovu dhidi ya Serikali, badala yake watoe ushauri na maoni ya kuibua hoja na changamoto zinazowakabili wananchi ili zitafutiwe ufumbuzi.”, alisema Mwenyekito huyo Mohamed Kawaida.
Alisema Serikali inaendelea kufanya mambo mengi ya maendeleo kwa nia ya kumaliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Mijini na Vijijini.
Mohamed Kawaida ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, alifafanua kuwa Makubalino ya Uwekezaji baina ya kampuni ya DP World na Bandari ya Dar es saalam una maslahi makubwa ya kuimarisha uchumi wa nchi.
Mohamed, alisema utatuzi wa kero na changamoto za Wananchi Mijini na Vijijini ndio kielelezo cha ushindi wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Naye Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa Mussa Haji Mussa, aliwasihi wananchi wa Mkoa huo kupuuza upotoshaji unaofanywa na Chama cha ACT-Wazalendo wa kudai kuwa Mkoa huo umetelekezwa na hauna maendeleo.
Nao Wajumbe wa Kamati tekelezaji ya UVCCM Taifa wakiwemo Wabunge,Wawakilishi na Wajumbe wa NEC kutoka katika Umoja huo walisema Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zimetekeleza kwa ufanisi Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025.