BAADHI ya Waalikwa na wanafunzi wa kituo hicho wakisikiliza nasahas mbali mbali kutoka kwa viongozi wa JImbo la Jang’ombe.
KATIBU wa Kamati Maalumu ya NEC,idara ya Organazesheni CCM Zanzibar ndugu Cassian Galos Nyimbo akihutubia wananchi katika uzinduzi wa Kituo cha ujasiriamali Jang’ombe.
MWAKILISHI wa Jimbo la Jang’ombe Mhe.Ramadhani Hamza Chande,akizungumza katika hafla hiyo
KATIBU wa Kamati Maalumu ya NEC,idara ya Organazesheni CCM Zanzibar ndugu Cassian Galos Nyimbo(wa pili kutoka kulia),akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Kituo cha mafunzo ya ujasiriamali cha Jimbo la Jang’ombe,Mwakilishi wa Jimbo hilo Mhe.Ramadhan Hamza Chande( wa kwanza kushoto) na Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Jimbo hilo ndugu Ali Ahmad Ibrahim(wa kwanza kutoka kulia).
**********************************
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
KATIBU wa Kamati Maalumu ya NEC,idara ya Organazesheni CCM Zanzibar ndugu Cassian Galos Nyimbo,amewataka Wanawake na Vijana wa jimbo la jang’ombe kutumia vizuri fursa ya ujasiriamali kwa kujiajiri wenyewe.
Wito huo ameutoa wakati akizindua Kituo cha Mafunzo ya Ujasiriamali cha Jang’ombe kilichoanzishwa na Mwakilishi wa Jimbo hilo uko Kilimani Mnara wa mbao Unguja.
Alisema ujasiriamali ni kazi kama zilivyo kazi zingine katika jamii hivyo ujuzi unaotokana na sekta hiyo unatakiwa kuthaminiwa na kupewa kipaumbele.
Galos alieleza kuwa mafunzo hayo ya ujasiriamali watakayopewa wananchi wa jimbo hilo kupitia Kituo hicho yawe na tija ya kujikwamua kichumi na kujiongezea kipato.
Katika maelezo ya Katibu huyo, alimpongeza Mwakilishi huyo kwa ubunifu wake wa kuanzisha Kituo kitakachozalisha wataalumu wengi wa masuala ya ujasiriamali wenye uwezo wa kutengeneza bidhaa mbali mbali zenye viwango.
“Nakuombeni hiki kituo mkitumie vizuri kwani mkipata ujuzi wa masuala ya ujasiriamali mtakuwa mmejikomboa katika wimbi la umaskini na kuwa na uwezo wa kujiajiri wenyewe.”, alisema ndugu Galos.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Jang’ombe Mhe.Ramadhani Hamza Chande,alisema lengo la kuanzisha kituo hicho ni kuwapatia ujuzi wa masuala ya ujasiriamali wananchi wa jimbo hilo hasa vijana na wanawake.
Alisema wakati akiomba kura za wananchi wampatie ridhaa ya uongozi aliahidi kuanzisha kituo hicho na kwa sasa ametekeleza ahadi hiyo.
Alisema katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020 imeelekeza uanzishwaji wa vituo vya mafunzo ya ujasiriamali nchini, hivyo jimbo hilo wametekeleza maelekezo ya Ilani.
Alisema kituo kimesajiliwa na kupitia taratibu zote za kisheria pia wana wakufunzi waliobobe katika kufundisha utengenezaji wa bidhaa bora zinakubalika katika soko la ndani na kimataifa.
Akitoa shukrani katika hafla hiyo Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mjini ndugu Kamaria Suleiman Nassor, aliwapongeza viongozi wa jimbo la Jang’ombe kwa ushirikiano wao uliozaa matunda ya kuanzisha kituo hicho kitakachowanufaisha Vijana.
Alisema vijana wa jimbo hilo wanatakiwa kuchangamkia fursa hiyo kwa kujiunga kituo hicho ili wapate ujuzi utakaowawezesha kutengeneza bidhaa zitakazowapatia kipato.