Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na wananchi na walengwa wa TASAF wa Kijiji cha Mwanangwa mara baada ya kukagua Shule ya Sekondari ya Wasichana Mwanangwa iliyojengwa kwa ufadhili wa TASAF, wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza. |
Mwonekano wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Mwanangwa iliyojengwa kwa ufadhili wa TASAF katika Kijiji cha Mwanangwa, Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza. |
Na. Veronica E. Mwafisi-Misungwi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewapongeza Viongozi na Wananchi wa Kijiji cha Mwanangwa kwa kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo kikamilifu baada ya kuridhishwa na thamani ya fedha iliyotumika katika mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Mwanangwa iliyojengwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.
Mhe. Simbachawene ametoa pongezi hizo alipokuwa akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na wananchi wa Kijiji cha Mwanangwa, Kata ya Mabuki katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza wakati wa ziara yake ya kikazi katika halmashauri hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa shughuli za TASAF.
“Nimefurahi sana na niwapongeze kwa kusimamia kikamilifu mradi huu wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Mwanangwa uliogharimu takribani shilingi milioni 168 kupitia fedha za TASAF, nimekagua na kuona majengo yote yalivyojengwa kwa ufanisi mkubwa, nimeridhika na thamani ya fedha ambayo imetumika hapa,’’ Mhe. Simbachawene amesema.
Aidha, Mhe. Simbachawene amewapongeza na kuwashukuru wananchi wa Misungwi kwa kuchangia nguvu zao katika kufanikisha ujenzi huo, hali inayoonyesha jamii pia imeshiriki kikamilifu katika ujenzi wa shule hiyo itakayowasaidia wanafunzi wa kike kupata elimu bora.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Mhe. Paulo Chacha amemshukuru Waziri Simbachawene kwa kufanya ziara katika Wilaya yake na kuahidi kuwa watumishi na wananchi wa Wilaya yake wataendelea kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano mkubwa ili kuleta maendeleo katika nchi.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Misungwi, Mhe. Alexander Mnyeti amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwapatia fedha za miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi na vituo vya afya katika jimbo la Misungwi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba na Misungwi mkoani Mwanza iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF pamoja na kuzungumza na watumishi wa umma kwa lengo la kutatua kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi wa halmashauri hizo.