Meneja Mawasiliano Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Bi. Subira Kaswaga, ametoa wito kwa taasisi za umma kujiunga na mfumo wa ubadilishanaji taarifa serikalini (GovESB) ili taasisi hizo ziweze kuwasiliana na kubadilishana taarifa kidijitali kupitia mfumo huo.
Kaswaga ametoa wito huo leo wakati alipofanya mkutano na waandishi wa Habari mkoani Mbeya, kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na e-GA kwenye maonyesho ya wiki ya wakulima ambayo kwa mwaka huu yanafanyika kitaifa jijini humo.
Alisema kuwa, mfumo wa GovESB ni shirikishi na unaziwezesha taasisi za umma kuunganisha mifumo yao ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kupitia mfumo huo ili kuweza kuzungumza na kubadilishana taarifa kidijitali.
Faida za mfumo huo ni pamoja na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika taasisi za umma, kuokoa muda, gharama za uendeshaji wa taasisi pamoja na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa wakati, alifafanua.
βMfumo wa GovESB ni jitihada za Mamlaka za kuhakikisha mifumo ya TEHAMA katika taasisi za umma inazungumza na kubadilishana taarifa ili kupunguza urudufu wa mifumo serikalini, kwa sasa taasisi mbalimnbali za umma zimeunganisha mifumo yake na GovESB lakini zipo taasisi ambazo bado hazijaunganisha, hivyo nitoe wito kwa taasisi hizo kujiunga na mfumo huu wa GovESBβ, alisema Kaswaga.
Alibainisha kuwa, e-GA imedhamiria kuhakikisha utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao katika taasisi za umma unaimarika ili kuhakikisha taasisi za umma zinatumia TEHAMA kwenye utendaji kazi wake na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha, aliongeza kuwa e-GA hushirikiana na taasisi nyingine za umma katika kutengeneza mifumo ya TEHAMA inayotumika katika taasisi hizo ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika taasisi na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
βMamlaka imedhamiria kuhakikisha kuwa, mwananchi anapata huduma zote za serikali kidijitali mahali alipo, ili kufikia malengo hayo, tunashirikiana na taasisi mbalimbali za umma kutengeneza mifumo ya kisekta itakayosaidia utendaji kazi katika taasisi hizo na kuwasaidia wananchi kupata huduma kidijitaliβ, alisisitiza.
Naye Afisa TEHAMA wa e-GA Bw. Caesar Mwambani alisema kuwa, Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa kushirikiana Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imetengeneza mfumo wa e-Mrejesho unaowawezesha wananchi kuwasiliana na serikali kidijidati.
Alisema kuwa, mfumo huo unawawezesha wananchi kuwasilisha maoni, changamoto, pongezi au malalamiko kwenda katika taasisi yoyote ya umma na kisha kufuatilia utekelezaji wake kwa njia ya kidijitali.
βMfumo huu unamrahisishia mwananchi kuwasiliana na serikali kidijitali na hivyo kumpunguzia gharama za kusafiri kwenda katika taasisi husika ili kuwasilisha kero yake na badala yake anaweza kuwasiliana na taasisi hiyo kupitia mfumo wa e-Mrejesho popote alipoβ, alisema.
Aliongeza kuwa, mfumo wa e-Mrejesho unapatikana kupitia tovuti ya www.emrejesho.go.tz, simu janja kwa kupakua aplikesheni yake au kwa namba ya msimbo kwa kupiga *152*00# na kisha atachagua namba 9, kisha namba 2 na kuwasilisha hoja yake kwenye taasisi husika.
Mamlaka ya Serikali Mtandao imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya 2019 ikiwa na jukumu la kuratibu na kusimamia utekelezajia wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao katika taasisi za umma.