Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) akifungua mafunzo ya mfumo mpya wa “Ajira Portal” kwa Maafisa Rasilimaliwatu serikalini yaliyofanyika jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya mfumo mpya wa “Ajira Portal” wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Dodoma.
Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi akifafanua changamoto za mifumo ya awali ya uombaji kazi, kabla ya ufunguzi wa mafunzo ya mfumo mpya wa “Ajira Portal” kwa Maafisa Rasilimaliwatu jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ACP Ibrahim Mahumi akizungumza kabla ya ufunguzi wa mafunzo ya mfumo mpya wa “Ajira Portal” kwa Maafisa Rasilimaliwatu jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi wa serikali baada ya kufungua mafunzo ya mfumo mpya wa “Ajira Portal” kwa Maafisa Rasilimaliwatu jijini Dodoma. Wengine ni Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi (kulia) na Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ACP Ibrahim Mahumi (kushoto).
***********************************************
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) amewataka waajiri
nchini kuhakikisha wanautumia vizuri mfumo wa “Ajira Portal” ili kukabiliana
na changamoto ya upendeleo wa ajira serikalini.
Mhe. Mkuchika ameyasema hayo, alipokuwa akizindua mafunzo kuhusu
mfumo mpya wa “Ajira Portal” kwa Maafisa Rasilimaliwatu serikalini jijini
Dodoma.
Mhe, Mkuchika amesema mfumo mpya wa “Ajira Portal” utaongeza ufanisi
katika suala la ajira kwani umeundwa ili kurahisisha mchakato wa ajira kati
ya Sekretarieti ya Ajira, waombaji wa kazi na waajiri serikalini.
“Matumizi sahihi ya mfumo huu yataongeza ufanisi, yatapunguza siku za
kuendesha michakato ya ajira na yatamwezesha mwajiri kutuma kibali
chake kupitia mtandao na kuweza kufuatilia maendeleo ya kibali cha ajira
kupitia mtandao” Mhe. Mkuchika amefafanua.
Mhe. Mkuchika ameongeza kuwa, mfumo huu pia utafikisha majina ya
waombaji wa ajira waliofaulu usaili kwa waajiri wote nchini siku hiyohiyo
yanapotumwa na Sekretarieti ya Ajira.
Amesema kuwapo kwa mfumo wa “Ajira Portal” kutaifanya serikali
iondokane na kasumba ya kuajiri watu wanaodanganya sifa zao halisi kwa
kuwa mfumo huo umewezeshwa kuongea na mifumo mingine mikubwa ya
utambuzi nchini ikiwemo NIDA, NACTE na NECTA.
“Sitafurahishwa na sitapenda kupata taarifa kwamba bado kuna waajiri
katika sekta ya umma hawatumii mfumo huu unaodhibiti vitendo vya
upendeleo na unaookoa muda wa mchakato wa ajira serikalini” Mhe.
Mkuchika amesema.
Akizungumza kwa Niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ACP Ibrahim Mahumi amesema kwa
mujibu wa tafiti aliyoifanya, Tanzania ni nchi pekee kwenye ukanda wa
Afrika Mashariki na Kati inayoongoza kwa kuwa na mfumo wa “Ajira
Portal”.
Awali, akitoa maelezo ya mfumo, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika
Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi amesema Sekretarieti ya Ajira
imeamua kubuni mfumo mpya wa “Ajira Portal” ili kukabiliana na
changamoto zilizojitokeza katika mfumo wa awali zilizokuwa
zinachelewesha mchakato wa ajira serikalini.
Bw. Xavier amesema, Sekretarieti ya Ajira ilikuwa ikitumia magazeti, mbao
za matangazo, televisheni, redio na tovuti kutangaza nafasi za ajira
serikalini ambapo mifumo hiyo iliisababishia serikali hasara kwa kuwa
gharama nyingi zilitumika kutangaza ajira hizo.
Mafunzo ya “Ajira Portal’ kwa Maafisa Rasilimaliwatu serikalini
yamefanyika kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi wao na kuwawezesha
kuwa na taarifa sahihi za waajiriwa zinazowafikia kwa wakati.