Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi(katikati) akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Mahakama ya Tanzania(MAHAKAMA SACCOS) leo Oktoba 26, mwaka huu wakati akiwa mgeni rasmi wa kufungua mkutano huo, uliofanyika katika ukumbi namba moj uliopo Mahakama Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam. Kulia wa pili ni Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Edwin Protas na wa kwanza ni Makamu Mwenyekiti,Bi.Haluwa Kivuma. Kushoto wa pili ni Bi. Herodia Kambanga na wa kwanza kushoto ni Bi. Irene Ngowi wote ni Maafisa Ushirika kutoka Manispaa ya Ilala.
Baadhi ya wanachama wa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Mahakama ya Tanzania (MAHAKAMA SACCOS) wakiwa kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka, uliofanyika leo, uliofanyika katika ukumbi namba moj uliopo Mahakama Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam.
(Picha na Magreth Kinabo – Mahakama)
……………………….
Na Magreth Kinabo- Mahakama
Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amewashauri viongozi na wanachama wa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Mahakama ya Tanzania(MAHAKAMA SACCOS) kukinadi chamam hicho ili kiweze kuwa na idadi kubwa ya wanachama na kuiwezesha Mahakama kuwa Taasisi bora inayoongoza kwa utoaji kwa riba nafuu kitaifa na kimataifa.
Akizungumza leo Oktoba 26, mwaka huu wakati akiwa mgeni rasmi wa kufungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa chama hicho, uliofanyika katika ukumbi namba moj uliopo Mahakama Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam, Jaji Kiongozi alisema ni vema viongozi hao na wanachama kuweka mikakati ya kuweza kuongeza idadi ya wanachama ili kufikia azima hiyo.
Alisema idadi ya majaji saba waliojiunga na chama hicho, bado ni ndogo, wakiwemo mahakimu na wasajili.
“Mnapaswa kuweka mikakati ya kukinadi chama hiki ili kuweza kuwa na angalau nusu ya idadi ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania, chama hakijafanyiwa uhamasishaji wa kutosha, hivyo kila mwanachama anaowajibu wa kuhamasisha watu kujiunga,” alisema Jaji Kiongozi.
Jaji Kiongozi aliongeza kwamba chama hicho, kinatakiwa kutumia mitandao ya kijamii na tovuti ya Mahakama ili kiweze kufahamika na kutangaza shughuli za kupitia mitandao hiyo, ikiwemo kuwa na vijarida na vipeperushi vya chama, kwa kuwa ni nyezo za kukifanya kiweze kufahamika.
Aidha Jaji Kiongozi alikishauri chama hicho, kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika shughuli zake, ikiwa ni hatua ya kuweza kuwafikia watumishi wengi na kupunguza gharama za uendeshaji.
Dkt. Feleshi alisema pia chama hicho, kitumike kama sehemu ya kudumisha, amani, upendo, ushirikiano na mshikamano miongoni kwa watumishi hao ili kiweze kusaidia changamoto za kiuchumi na kijamii hali itakayosaidia wanachama kuweza kufanya kazi za utoaji haki kwa hisia.
Awali akizungumza kabla ya kukaribisha, Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Edwin Protas alisema kilianzishwa mwaka 1970 kikiwa na wanachama 84 na hivisasa kina wanachama 372, kati ya watumishi zaidi ya 5000 wa Mahakama.
Protas alisema kwamba baadhi wanachama wake, ambao si maafisa wanakabiliwa na changamoto ya kuwa na mishahara midogo, hivyo aliiomba Tume ya Utumishi ya Mahakama ya Tanzania kuweza kuliangalia suala hilo, ili chama kisiweze kuzorota.
Kwa upande wake, Afisa Ushirika kutoka Manispaa ya Ilala,Bi. Herodia Kambanga alikitaka chama hicho kuwa ushirikiano na vyama vingine ili kuweza kubadilisha uzoefu na kutatua changamoto mbalimbali.