Mkufunzi Dkt.Kijakazi Ali Makme akizungumza na walimu na wanafunzi wa vyuo mbalimbali wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo washiriki hao juu ya Mbinu za Kufundishia lugha ya kiswahili kwa Wageni,hafla iliyofanyika Julai 31,2023 huko Ofisi za Bakiza Mwanakwerekwe Zanzibar.
Baadhi ya Washiriki wa mafunzo ya kuwajengea uwezo juu ya mbinu za kufundisha lugha ya Kiswahili kwa Wageni wakifuatilia mafunzo hayo yaliyofanyika Ofisis za Baraza la Kiswahili Mwanakwerekwe Zanzibar Julai 31,2023 huko Ofisi za Bakiza Mwanakwerekwe Zanzibar.PICHA NA FAUZIA MUSSA -MAELEZO ZANZIBAR
Na Rahma Khamis Maelezo
Katibu Mtendaji Baraza la Kiswahili Zanzibar Dkt Mwanahija Ali Juma amewataka walimu wanaomaliza mafunzo ya kiswahili kwa wageni kufuatilia fursa zinazojitokeza ndani na nje ya nchi ili kuleta maendeleo.
Akizungumza na wanahabari mara baada ya kufungua mafunzo kwa walimu hao juu ya mbinu za kufundishia wageni huko Ofisini kwake Mwanakwerekwe Wilaya ya Magharibi B, amesema fursa za ajira kupitia lugha ya kiswahili zimekua kwa kasi kubwa hivyo kupitia mafunzo hayo yatasaidia katika kuzipata fursa hizo.
Amesema kuwa lengo mafunzo hayo ni kuwafanya walimu kuweza kuzitendea haki fursa zilizopo ndani ya lugha ya kiswahili na kukieneza kiendelee kutumika duniani kote.
Aidha amefahamisha kuwa Baraza la Kiswahili limekuwa likitoa mafunzo kama hayo mara kwa mara kwa walimu mbalimbali wa lugha ya kiswahili ili kuweza kuikuza zaidi lugha hiyo na kupata fursa kwa wageni wanaotaka kujifunza .
“Tunawafundisha walimu juu ya mbinu za kufundishia wageni mara kwa mara na hii ni awamu ya tatu mara ya kwanza tulifundisha Unguja ,awamu ya pili Pemba na hii mara ya tatu tumefundisha hapa tena ili tuwe na walimu wazuri wenye uwezo wa kufundishia wageni wetu,” alifafanua Katibu .
Dkt Mwanahija ameeleza kuwa mafunzo hayo yanatolewa kwa walimu wa ngazi ya shahada ya kwanza ambao tayari wamejifunza lugha hiyo na wana uelewa wa muda mrefu .
Hata hivyo Dkt ameongeza kwa kusema kuwa wanatarajia kuwa na walimu wa kutosha kwani kuna wageni wengi wanaotaka mafunzo ya lugha hiyo na kuwashauri walimu hao kushirikiana kwa pamoja ili kufikia lengo.
Nae Mkufunzi wa mafunzo hayo Zainabu Ali Iddi amesema kuwa wamejipanga kutoa mafunzo ya shahada ya kwanza kwa lengo la kukabiliana na soko la lugha ya kiswahili kwa vile kinatumika katika nchi nyingi ulimwenguni.
Amesema taaluma yeyote inahitaji ujuzi hivyo wanatoa elimu ili kukabiliana na wageni wanaotaka kujifunza kwa kutumia mbinu za kisasa zaidi.
Aidha amefahamisha kuwa wakati watakapomaliza mafunzo hayo watakuwa na ununuzi wa kutosha pamoja na kuingiwa na hamasa ya kujifunza zaidi katika kubuni mbinu zaidi za kufundishia .
Nae Mratibu wa Mafunzo ya Baraza la Kiswahili Daulat Abdalla Said amesema kuwa ni jambo la kufurahisha kuona awamu hiyo watu wengi wamehamasika na wamejitokeza kushiriki mafunzo hayo .
” Kuna wanafunzi wengine wamekuja kwa ajili ya kujifunza ambao wanatoka udom na mwalimu Nyerere mbapo kuna walimu wa kiswahili hii inaonesha jinsi gani wamehamasika zaidi ” ameeleza Mratibu .
Nao washiriki wa mafunzo hayo wamesema ni jambo jema na muhimu kupatiwa mafunzo hayo kwani yatawawezesha kupata fursa zaidi kutokana na ukuwaji wa lugha hiyo.
Aidha wamefahamisha kuwa iwapo watapata mafunzo hayo wataweza kupata fursa nyingi katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi ili kujiongezea kipato kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Jumla ya washiriki 100 wamepatiwa mafunzo juu ya mbinu za kufundishia wageni kutoka Vyuo mbalimbali ikiwemo Chuo kikuu cha Zanzibar ZU,Chuo Kikuu cha Dodoma UDOM , ,Mwalimu Nyerere Bububu na Abdulrhman Alsumeit Chukwani.