Bunge Wa Jimbo La Manonga Seif Hamisi Gulamali Akisalimiana Na Jilunga Ngoho Mkazi Wa Kijiji Cha Ngulu Baada Ya Kuwasili Katika Kata Ya Ngulu Ikiwa Ni Mwisho Wa Ziara Yake Katika Jimbo La Manonga.
Mbunge Wa Jimbo La Manonga Seif Hamisi Gulamali Wa Nne Kutoka Kushoto Akiwa Na Viongozi Wa Kijiji Cha Mwasunghu Kata Mwashiku Wakienda Kukagua Daraja.
Na Lucas Raphael,Tabora
Mbunge wa Jimbo la Manonga Wilaya ya Igunga mkoa wa Tabora Seif Khamisi Gulamali amewataka wa wananchi wa wailaya hiyo kujenga nyumba bora katika maeneo yao zitakazowasaidia kujikwamua kiuchumi kwa kupangisha watumishi
Akizungumza na wananchi wa kata ya Mwashiku kijiji cha Matinje na kata Ngulu kijiji cha Ngulu, Gulamali alisema pamoja na juhudi za Serikali za kuwekeza miundominu ya elimu, afya, maji, barabara, umeme katika vitongoji, vijiji, kata kwa kiasi kikubwa lakini amebaini bado kuna changamoto kubwa ya nyumba za watumishi hali ambayo inalazimika watumishi wengi kuishi mbali na vituo vyao vya kazi.
Kufuatia hali hiyo Mbunge huyo aliwashauri wananchi wa Jimbo la Manonga kutumia fedha zao wanazozipata kupitia kilimo , ufugaji na madini kuwekeza kwa kujenga nyumba bora katika maeneo yao watakazowapangisha watumishi na kujiingizia kipato cha kila mwezi kwa kuwa Serikali imefikisha miundombinu katika maeneo yao.
“Ndugu zangu wananchi mimi kama Mbunge wenu mlienichagua naomba niwape ushauri, changamoto nilioiona katika ziara yangu kwa baadhi ya maeneo nimebaini watumishi wa Idara mbalimbali ikiwemo afya hawakai katika vituo vyao vya kazi hivyo sio kosa lao bali ni ukosefu wa nyumba za watumishi hivyo wananchi naomba muiunge serikali mkono kwa kujenga nyumba bora katika maeneo yenu kwani hizo mtapangisha wenyewe” alisema Gulamali.
Wakati huo huo Gulamali akifanya Majumuisho ya ziara yake katika ukumbi wa mkutano ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Igunga na wakuu wa Idara wakiongozwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Igunga Athumani Msabila na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Igunga.
Mbunge huyo alibainisha kuwa baadhi ya maeneo mengi aliopita wananchi wamekuwa wakiwalalamikia baadhi ya viongozi kutotimiza majukumu yao vizuri ikiwemo kutosoma mapato na matumizi kwa wananchi kwa muda mrefu, kuchangisha michango pasipo kutoa risiti na majibu yasiyoridhisha kwa baadhi ya watumishi wa idara ya afya katika zahanati na vituo vya afya.
Alisema kero zingine alizobaini ni fedha zinazolewa na serikali za miradi ikiwemo ujenzi wa majengo ya shule, zahanati kuliwa hovyo huku akitolea mfano katika kijiji cha Ikunguipina mifuko 40 ya simenti ilitolewa na fedha za mfuko wa Jimbo la Manonga kwa ajili ya ujenzi wa zahanati kuharibika pasipo kutumika.
Aidha baadhi ya kero zingine ni askari wasio waadilifu katika mnada wa kata ya Iborogero unaofanyika kila jumatatu ya wiki kuwakamata wananchi wanaotoka vijijini na kuwaomba rushwa ya sh. 20,000 hadi 50,000 na wanapodai risiti hupewa vitisho ambapo askari hao huacha ulinzi katika mnada huo na kuenda nje kidogo kuwavizia wananchi hao.
Kutokana na hali hiyo Mbunge Gulamali aliwaomba viongozi wote ambao idara zao zimelalamikiwa na wananchi kufuatia kwa karibu na kutatua kero hizo ambazo ziko ndani ya uwezo wao ikiwa ni moja ya kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassani kwa kuzuia upigaji wa fedha anazotoa kwa wananchi wake.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Igunga Athumani Msabila alisema atafuatilia mapungufu yote aliyoyabaini Mbunge katika ziara yake na kuongeza kuwa fedha zote zinazotolewa na Rais Samia Suluhu Hassani atazisimamia kwa uadilifu mkubwa kwa shughuli iliyokusudiwa na kumpongeza kwa kazi nzuri ambazo amekuwa akifanya hapa nchini.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora Kamishina msaidizi Richard Abwao alisema baadhi ya askari waliolalamikiwa wakati wa ziara ya Mbunge Seif Hamisi Gulamali atafuatilia kwa karibu kuhusu tuhuma hizo na watakaobainika atachukua hatua za kisheria.
Katika ziara ya mbunge huyo alitembelea kata 19, vijiji 63 pamoja na kufanya mikutano ya hadhara na kusikiliza kero za wananchi .