SERIKALI ya Tanzania imelaani vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Serikali ya Marekani dhidi ya Cuba na Zimbabwe kwa sababu vinadhoofisha biashara, uwekezaji na ustawi wa wananchi na imetaka vikwazo hivyo viondolewe.
Tamko hilo limetolewa leo (Jumamosi, Oktoba 26, 2019) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye Mkutano wa 18 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) ulioanza leo huko Baku, Azerbaijan.
“Vizuizi na vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa dhidi ya Cuba na Zimbabwe vinadhoofisha maendeleo ya uchumi, uwezo wa kufanya biashara, fursa za uwekezaji na ustawi wa wananchi wake.”
“Tanzania inaungana na Jumuiya ya Kimataifa kutaka yawepo majadiliano ya msingi ambayo yataondoa vizuizi kwa Serikali ya Cuba na vikwazo kwa Serikali ya Zimbabwe ili kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa manufaa ya watu wa nchi hizo,” amesema.
Mwaka 2001, Marekani na Jumuiya ya Ulaya (EU) ziliweka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Zimbabwe baada ya Serikali ya nchi hiyo chini ya uongozi wa Rais Robert Mugabe kuamua kuchukua ardhi yote iliyokuwa ikimilikiwa na wageni.
Waziri Mkuu ambaye anahudhuria mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, aligusia mambo kadhaa ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, masuala ya Sahara Magharibi, usalama wa Palestina na msimamo wa Tanzania kwenye Umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM).
Kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, Waziri Mkuu amesema suala hilo ni mojawapo ya changamoto kubwa zinazoikabili dunia na wanadamu kwa sasa. “Tunaiomba Jumuiya ya Kimataifa iweke njia muafaka ambazo zitasadia kurekebisha tishio ambalo tunakabiliana nalo hivi sasa. Tunazitaka nchi zilizoendelea zitimize ahadi zao na michango ya kifedha, zisaidie kujenga uwezo na kutoa wataalamu watakaozisaidia nchi zinazoendelea,” amesema.
Akizungumzia Sahara Magharibi, Waziri Mkuu amesema suala la kujitawala kwa nchi hiyo limeingia sura mpya baada ya Morocco kujiunga tena na Umoja wa Afrika na kwamba hivi sasa imekuwa mjumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
“Ipo fursa kubwa hivi sasa kwa Umoja wa Mataifa pamoja na mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ya kuweza kushirikiana na chombo kipya cha Troika kilichoundwa na Umoja wa Afrika katika kuliangalia suala zima la Sahara Magharibi. Tanzania inaunga mkono jitihada hizo,” amesema Waziri Mkuu.
Kwenye suala la Palestina, Waziri Mkuu amesema Tanzania inatambua kwamba nchi hiyo ina haki ya kufurahia amani na uhuru wake kama ilivyo kwa Israeli, kwa mujibu wa mkataba wa Umoja wa Mataifa. “Ni matumaini yetu kwamba kuendelea kuwepo kwa jitihada za kimataifa, mgogoro huo utapatiwa ufumbuzi katika muda muafaka na mataifa haya mawili yataishi kwa amani na utulivu.”
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuelezea msimamo wa Tanzania kwenye umoja huo na kusisitiza kwamba Tanzania bado ina imani na chombo hicho. “Tanzania itaendelea kuheshimu kazi zinazofanywa na umoja huu kama ambavyo tumekuwa tukifanya kwa miaka 58 iliyopita. Tunaomba ushirikiano baina ya nchi za Kusini uimarishwe. Ushirikiano baina ya nchi zinazoendelea na zilizoendelea nao pia uimarishwe.”
Amesema: “Serikali ya Tanzania inapongeza uhusiano ulipo baina ya Umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM), kundi la nchi 77 (G77) na China na kwamba tunatamani ujizatiti zaidi kutetea maslahi ya umoja huu ambao wanachama wake wengi ni nchi zinazoendelea.”
Waziri Mkuu Majaliwa ameambatana na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika ya Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro na Balozi wa Tanzania nchini Urusi ambaye pia ni Balozi wa Azerbaijan, Meja Jenerali Mstaafu, Simon Mumwi.