Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze
Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Mkoa wa Pwani, amesema Serikali imeinusuru shule ya msingi Mwalivundo kwa kupeleka fedha kujenga madarasa,choo kwa gharama ya zaidi ya milioni 120 ,shule ambayo ilikuwa kwenye hatari ya kufungwa kutokana na ukosefu wa miundombinu bora.
Akiwa kwenye muendelezo wa ziara yake jimboni, kijiji Cha Mwalivundo, ameeleza ,Serikali imepeleka sh.milioni 100 kujenga madarasa 5 shuleni hapo na choo kwa gharama ya sh.milioni 20.
Pamoja na hayo Serikali imetenga kiasi cha sh.milioni 50 kumalizia ujenzi wa zahanati ya Mwalivundo.
“Tunapenda kuishukuru Serikali chini ya Rais wetu SSH kwa fedha za miradi zilizochangia ujenzi huu wa madarasa matano na vyoo katika shule ya msingi Mwalivundo, ambayo ilikuwa kwenye hatari ya kufungwa kutokana na ukosefu wa madarasa na vyoo vyenye ubora.”
“Napenda kuwashukuru wananchi wa kata ya Pera na Halmashauri ya Chalinze kwa ushirikiano na kazi kubwa inayoleta matunda makubwa, Nguvu ya wananchi nimeiona”
Ridhiwani ameelezea, shule imekamilika na watoto wanakwenda shule bila kuwa na changamoto zozote! Kwani huduma zote muhimu za kijamii zimeboreshwa.
Anaeleza Serikali imepeleka fedha nyingi kwenye miradi mbalimbali jimbo la Chalinze kama ilivyo maeneo mengine Nchini, na kueleza Kiukweli imefanya makubwa .
Pia mbunge huyo ,ameishukuru Serikali kwa kupeleka milioni 149 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto, kituo cha Afya Miono.
Katika hatua nyingine, Ridhiwani ametembelea kujionea maandalizi ya upanuzi wa kituo cha afya Miono, mradi wa ujenzi wa madarasa 6 na mabweni 4 katika Sekondari ya Miono na ameridhishwa na hatua iliyofikia miradi hiyo.
Ridhiwani aliwataka wananchi Chalinze, wasibweteke kuridhika na mafanikio yàliyopo bali waendelee kushirikiana ili kujiinua kimaendeleo na Uchumi.
Katika ziara hiyo ametembelea pia kitongoji Cha Machala kuona Zahanati inayojengwa pamoja na miradi ya maji, miundombinu ya mazingira ya wanafunzi (shule), kijiji cha Mihuga, Kikaro na Miono.