Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya uchechemzi kwa kamati za PETS kuhusu ushiriki na ushirikishwaji wa wananchi katika serikali za mitaa yaliyoendeshwa na Shirika lisilo la Kiserikali la ROA wilayani Songea.
Mwezeshaji wa mafunzo ya Uchechemzi kwa kamati za PETS kuhusu Ushiriki na ushirikishwaji wa wananchi katika serikali za mitaa Mnung’a Shaibu akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo yaliyofanyika jana mjini Songea.
Mwanasheria ambaye pia ni mjumbe wa PETS James Simon, akitoa mada kwa washiriki wa mafunzo hayo kuhusiana na mchango wao katika kuisaidia jamii kuelewa masuala mbalimbali ikiwemo miradi ya maendeleo inayoibuliwa na kutekelezwa katika maeneo yao.
Na Muhidin Amri,
Songea
WITO umetolewa kwa viongozi wa na watumishi wa umma nchini,kuacha tabia ya kukumbatia madaraka wanapoanza michakato ya kuibua na kutekeleza miradi ya maendeleo yenye lengo la kuboresha huduma za kijamii na kupunguza kiwango cha umaskini hapa nchini.
Badala yake wameombwa kuishirikisha jamii kwa kila hatua,ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa wakati na kuharakisha kukua kwa uchumi hasa katika maeneo ya pembezoni.
Hayo yamesemwa jana na Mshauri mwelekezi(Consultant) wa masuala ya Utawala bora na uwajibikaji Mnung’a Shaibu wakati wa mafunzo ya kuzijengea uwezo kamati za Pets kuhusu ushiriki na uwajibikaji wa wananchi katika serikali za mitaa.
Mafunzo hayo ya siku mbili yamefanyika katika chuo cha Top One mjini Songea, yamelenga kuwajengea uelewa washiriki hao kuhusu Dhana ya utawala bora,haki na wajibu na ushiriki wa wananchi katika serikali za mitaa,vitongoji na vijiji hapa nchini.
Mnung’a alisema,suala ushirikishwaji katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kati ya jamii na viongozi ni jambo muhimu kwani linasaidia miradi kutekelezwa kwa ubora na kwa wakati sahihi na wananchi wanakuwa sehemu ya walinzi wa miradi hiyo.
Alieleza kuwa,uzoefu unaonyesha miradi mingi inayotekelezwa kwa kuishirikisha jamii imefanikiwa kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na ambayo imetekelezwa na upande mmoja wa serikali tena kwa gharama kubwa.
“kuna tabia inayoendelea viongozi wa serikali waliopewa dhamana ya kusimamia shughuli na miradi ya maendeleo katika maeneo yetu kutumia mabavu na maamuzi binafsi kwenye utekelezaji wa miradi,hali ambayo imesababisha baadhi ya miradi kutokamilik kwa wakati”alisema.
Ametoa wito kwa jamii wakiwemo wajumbe wa mradi PETS, kuisaidia serikali katika kuibua na kushiriki kikamilifu ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao badala ya kubaki nyuma.
Aidha,amewataka wajumbe wa mradi wa PETS kuwa na tabia ya kujisomea na kujifunza mambo mbalimbali ili kuwa na uelewa wa kutosha wanapokwenda kufuatilia ubadhilifu wa rasilimali za umma na miradi inayotekelezwa katika maeneo yao.
Naye Mshauri wa masuala ya sheria wa Roa James Simon,amewataka washiriki wa mafunzo hayo kwenda kuwasaidia wananchi kufahamu mapato na matumizi,fedha zinazokusanywa na miradi inayopelekwa katika vijiji vyao.
Amewaomba kwenda kuwa sehemu ya jamii na kushiriki katika hatua zote za utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo na kuepuka kuwa kikwazo kwa kukwamisha mipango mbalimbali iliyowekwa na serikali iliyopo madarakani.