Bwana Shamba Aman Abdulla Kambi akizungumza na wakulima kuhusiana na mbegu bora za matunda na mbogamboga huko Ukumbi wa Maleria Mwanakwerekwe Zanzibar.PICHA NA FAUZIA MUSSA
Na Rahma Khamisi Maelezo.
Wakulima wa viungo na mbogamboga wametakiwa kuwatumia wataalamu wa mbegu na mazingira ili kuweza kufahamu namna gani wataweza kulima kilimo chenye tija.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Afisa fedha wa Miradi wa Viungo Agnes Nicodemus amesema kuwa wakulima wengi hawafahamu aina ya mbegu za kutumia kwa kuzingatia mazingira jambo linalowakosesha mazao yenye ubora.
Amesema lengo la kutoa elimu kwa wakulima hao ni kuwaunganisha wauza pembejeo na wakulima kwani kuna baadhi ya changamoto zinazotokana na udhaifu wa mbegu wanazotumia.
Aidha amefahamisha kuwa kuna baadhi ya maeneo yanakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa mbegu sambamba na mazingira hivyo amewataka wakulima hao kuchangamkia fursa za mafunzo ili kuweza kuzitatua changamoto hizo.
“unaweza kupanda mazao yakawa hayakutoka kutokana na hali ya mazingira yaliyopo na aina ya mbegu kuwa haichukuani jna mazingira yale hivyo ni bora kupata elimu kwaza hii itatusaidia kujua aina gani ya mboga tulime na katika mazingira gani “alieleza Afisa huyo
Nae Bwana shamba Aman Abdullah Kambi amewataka wakulima kutumia mbegu zinazoendana na mazingira ya ardhi sambamba na hali ya hewa ili kunufaika na kilimo hicho.
Aidha amefahamisha kuwa iwapo watatumia aina ya mbegu hizo wakulima hao wataweza kulima kilimo cha biashara na kujiongezea kipato kutokana na kufahamu zaidi jinsi ya kutumia aina bora ya mbegu.
Nao washiriki wa mkutano huo wamesema wamefurahi kupata elimu hiyo na kuahidi kuitumia kwa vitendo elimu hiyo ili kujiletea maendeleo.
Aidha wamesema awali walikua wakipata shida kutokana na kupanda mbegu bila ya kuzingatia mazingira jambo lililowapa usumbufu katika kilimo chao .
Hata hivyo wameomba kuendelea kupatiwa elimu kama hiyo mara kwa mara ili kuweza kulima kilimo chenye tija zaidi na kujipatia kipato wao wenyewe na taifa kwa ujumla .