Na.Alex Sonna,Dodoma
WANACHAMA wa chama cha mapinduzi (CCM) mtaa wa Muungano kata ya Nkuhungu jijini Dodoma wamegoma kurudia kupiga kura za maoni kuwachagua viongozi ambao watakiwakilisha chama hicho katika uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 24 mwaka huu.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini hapa wanachama hao wamedai kuwa hawarudii kupiga kura kama ambavyo uongozi wa CCM wilaya umeagiza.
Mmoja wa wanachama hao Tatu Said, alisema kuwa juzi walipiga kura na kumchagua kiongozi ambaye wanaona anaweza kuwaongoza katika mtaa huo kwa miaka mitano ijayo.
Said alisema kuwa katika uchaguzi uliofanyika ndani ya chama juzi Oktoba 20, mwaka huu walimchagua Nelson Mpolo kwa kura 81 dhidi ya mshindani wake Alli Mgwadu aliyekuwa mwenyekiti wa mtaa anayemaliza muda wake aliyepata kura 36.
“Tunashanga kuamabia leo tena tunatakiwa kurudia kupiga kura wakati yatari tulishachagua viongozi wetu na kura zilihesabiwa mbele ya watu wengine na wale walioshindwa walitia saini kukubari matokeo”alisema
Pia alisema kuwa wanachokishangaa zaidi ni kuona uongozi wa CCM ngazi ya wilaya kumbeba aliyekuwa Mwenyekiti baada ya kuonekana kuwa ameshindwa kutokaa na kura za wanachama.
“Kwanini viongozi wa wilaya walisimamie hilo suala na kusema kuwa mgombea huyu amekataa rufaa eti kwa madai kuwa uchaguzi hakuwa huru na haki sisi hatumtaki tena kutuongoza yeye kwanini anaendelea kung’ang’ania”alihoji.
Naye Mohamed Abubakari, alisema kuwa hata kama chama hicho kitambeba kiongozi huyo wao wataendelea kupiga kura za kumpinga kutoka na kushindwa kuwangoza kwa miaka mitano iliyopita.
“Sisi hapa tunachangamoto nyingi sana hatuma maji, barabara, shule lakini pia kwa miaka mitano ambayo amekuwa kiongozi wetu Alli Mugwadu hatujawahi kusomewa mapato na matumizi ndani ya muda wote huo”alisema
Akizungumza na waandishi waliofika katika eneo hilo Mwenyekiti wa CCM kata ya Nkuhungu, Nasoro Magari alisema kuwa wameamua kutangaza kurudiwa kwa uchaguzi huo kutokana na kupata maelekezo kutoka ofisi ya chama wilaya ya Dodoma mjini.
“Juzi tulifanya uchaguzi na hakukuwa na changamoto yoyote ile wagombea walioshindwa walikubari matokeo na kusaini karatasi za matokeo lakini jana nashaanga kupata taarifa kuwa kuna mgombea mmoja amekata rufaa kwa madai kuwa uchaguzi haukuwa wa haki”alisema
Mwenyekiti huyo wa CCM kata alisema pamoja na uongozi wa wilaya kutoa maagizo hayo lakini wao kama kata hawajaitwa ili kuhojiwa namna ambavyo uchaguzi ulikuwa.
Hatahivyo alisema kwa mujibu wa barua aliyoandikiwa na uongozi wa CCM Wilaya uchaguzi huo unatakiwa kuridiwa na wagombea wote waliochukua fomu majina yao yapelekwe kwa wanachama kwajili ya kupigiwa kura.