Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MKURUGENZI wa shirika la ALL FOR HIS GLORY, Dkt Israel Ole Gabriel Maasa ambaye ni Askofu wa Kanisa la Internation Evangelisim na Katibu wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania (JMT) ameikabidhi Serikali ambayo imejengwa kwa ushirikiano na Taasisi hizo za madhehebu mbalimbali.
Askofu Dkt Maasa ameikabidhi zahanati hiyo kwa Naibu Waziri wa Afya Dkt Godwin Mollel, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Dkt Suleiman Serera na Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, ili iweze kutumiwa na wananchi wa eneo la Nakweni Kata ya Shambarai.
Akizungumza wakati wa kukabidhi zahanati hiyo Askofu Dkt Maasa, amesema wameweza kufanikisha maendeleo hayo kwa ushirikiano na taasisi hizo za dini.
“Tunawashukuru wote waliofanikisha haya, akiwamo Mkurugenzi wa ALL FOR HIS GORY AFRICA Dkt Moris Odhiambo,” amesema Askofu Dkt Maasa.
Askofu Dkt Maasa, amesema pia wameweza kuchimba visima vitatu ambavyo vitatumiwa na wananchi wa Nakweni na mifugo yao katika kuwapatia maji.
Naibu Waziri wa Afya Dkt Godwin Mollel amemshukuru Askofu Dkt Maasa, kwa kuziongoza taasisi za dini katika kufanikisha ujenzi wa zahanati hiyo yenye manufaa makubwa kwa jamii.
“Tunawashukuru pia kwa kujenga jengo ambalo litaweza kutumiwa kuishi na watumishi wa zahanati hii huku wakilipia gharama kidogo,” amesema Dkt Mollel na kuongeza;
“Pia ninakushukuru Askofu Dkt Maasa kwa kulipa jina langu kisima kimoja ambacho wananchi wa hapa Nakweni na mifugo yao, watakuwa wanakunywa maji, japokuwa watu wataona ni jambo dogo ila kwa upande wangu ni kubwa mno.”
Ofisa mtendaji wa kijiji (VEO) cha Nakweni, Noel Mollel amesema wananchi wanamshukuru Askofu Dkt Maasa kwa kufanikisha ujenzi wa zahanati hiyo ambayo wananchi waliishia njiani kuijenga.
“Wananchi walijenga vyumba nane na kuishia hatua ya linta na shirika la ALL FOR HIS GLORY chini ya Mkurugenzi wake Askofu Dkt Maasa wakamalizia vikawa vyumba 15,” amesema Mollel.
Amesema zahanati hiyo itawanufaisha wananchi wa eneo hilo ambao walikuwa wanatembea umbali wa kilomita 12 hadi kituo cha afya Mirerani ili kupata huduma za afya.
Amemshukuru Dkt Maasa kwa kuwachimbia visima virefu vitatu, ambavyo vimekuwa mkombozi kwa wananchi na mifugo ya eneo hilo la kijiji cha Nakweni katika kupata maji.
“Tunamshukuru Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Dkt Suleiman Serera na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Dkt Aristidy Raphael kwa ushirikiano wao mkubwa waliotupatia kwa kipindi chote cha ujenzi wa zahanati hii,” amesema Mollel.