**********************************
Wasaidizi wa msaada wa kisheria mkoani Iringa wametaka kutambuliwa na vyombo mbali mbali vya kisheria kama polisi ,mahakama na magereza ili kuepuka kusumbuliwa pindi wanapotekeleza majukumu yao ya kuhudumia jamii .
Wakizungumza jana katika ukumbi wa siasa ni kilimo katika mdahalo wa siku moja juu ya sharia za msaada wa kisheria Tanzania ,utekelezaji wake ,changamoto na mafanikio yake , washiriki wa mdahalo huo walisema kuwa kutokana na kutotambuliwa kumekuwepo na usumbufu mkubwa kwa baadhi ya wasaidizi wa kisheria kukamatwa ama kuzuiliwa kutoa huduma katika jamii .
Msaidizi wa kisheria kutoka Halmashauri ya Mufindi Gabriel Nsemwa alisema kuwa wasaidizi hao wamekuwa wakishindwa kutimiza wajibu wao hasa pale wanapokutana na polisi katika maeneo ya wao kufuatilia matukio yanayohitaji msaada kutoka kwao .
Alisema kuwa mwezi uliopita msaidizi wa kisheria mwenzake kutoka wilaya ya Mufindi akiwa katika utekelezaji wa majukumu yao alikutana na polisi ambao walimkamata na kumpeleka kituo cha polisi na kukaa ndani kwa masaa nane .
“ Huyu alikamatwa usiku wakati akifuatilia tukio ambalo lilikuwa likihitaji msaada na akiwa eneo la tukio polisi nao wakiwa katika ufuatiliaji wa tukio hilo hilo walimkamata na kumpeleka kituoni Mafinga na kutozwa faini ya shilingi 230,000 na kukaa mahabusu masaa nane kuwa hawamtambui kama msaidizi wa kisheria hivyo tunataka kujua uhakika wa usalama wetu pindi tukiwa katika utekelezaji wa majukumu yetu “
Kuwa ili kuepusha kukamatwa kwa watoa huduma za kisheria na polisi ni vizuri chama cha mawakili Tanganyika kuangalia uwezekano wa kuwalinda ili wasiendelee kunyanyasika wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao .
Kwa upande wake mkaguzi msaidizi wa polisi Elizabeth Swai ambae alimwakilisha mkuu wa upelelezi wa polisi kwenye mdahalo huo alisema kuwa ni vizuri kwa wasaidizi hao wa kisheria na mawakili kufanya kazi kwa kufuata taratibu za sehemu husika badala ya kutaka kuingia hata maeneo ambayo hawapaswi kuingia bila ruhusa ya utawala wa eneo mfano mahabusu .
Kwani alisema wapo baadhi ya mawakili ama wasaidizi wa kisheria wamekuwa wakilamisha kuingia mahabusu kutaka kuongea na mahabusu bila kufuata taratibu jambo ambalo si sawa kwani kama watafuata taratibu hakuna askari atakayezuia wakili ama msaidizi wa kisheria kufanya mazungumzo na mahabusu .
Katibu mkuu wa shirika la LREO Jimmy Mgovano alisema kuwa ili kuepuka wasaidizi wa kisheria kutonyanyasika katika maeneo ya mahakama ,polisi ama magereza ni vizuri kukawa na orodha ya wasaidizi wa kisheria wote ndani ya mkoa ambao majina yao yatakuwepo kila eneo ili wakifika waweze kutambuliwa kwa orodha hiyo .
Mratibu wa chama cha mawakili mkoa wa Iringa Omary Sarehe alisema kuwa kila mwaka chama cha mawakili Tanganyika wamekuwa wakiandaa wiki ya msaada wa kisheria kwa ajili ya kuwatambua watu wenye uhitaji wa msaada wa kisheria katika vyombo vya kisheria hasa mahakamani .
Hivyo alisema kuwa ni vema serikali kuanzisha utaratibu wa kuandaa orodha ya wasaidizi wa kisheria wote ambayo itakuwepo kila idara ili kuepuka tasnia hiyo kuingiliwa na mawakili makanjanja.
Japo alisema kuwa upande wa mahakama wamepiga hatua kwa kuanzisha mfumo wa kimtandao ambao unatambua mawakili wote na wananchi wanaweza kukwepa kutapelewa na mawakili feki kwa kutembelea katika mtandao na kutafuta mawakili ambao wanatambulika