Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MBUNGE wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka ataanza ziara ya kutembelea Kata mbalimbali ili kuzungumza na kusikiliza kero za jamii na kukomesha maneno yanayosemwa kuwa huwa hafanyi ziara zake zaidi ya kudandia ziara za viongozi wenzake wanapotembelea Simanjiro.
Ole Sendeka akizungumza kwenye tukio la Naibu Waziri Dkt Godwin Mollel kukabidhi zahanati ya Kijiji cha Nakweni Kata ya Shambarai, iliyojengwa na taasisi ya ALL FOR HIS GLORY, amesema ataanza ziara zake hivi karibuni.
“Nitaanza kufanya ziara zangu na kuzungumza na watua kwenye maeneo mbalimbali ili tuwaeleze wananchi maendeleo yaliyofanyika, kuna baadhi ya watu wamekuwa wanazungumza hoja potofu yakuwa sizunguki jimboni,” amesema Ole Sendeka.
Mkazi wa Kata ya Endiamtu Mashaka Jororo amepongeza hatua hiyo ya Mbunge huyo Ole Sendeka kuanza ziara zake na kusikiliza kero za wapiga kura wake na kuelezea maendeleo mbalimbali yaliyofanyika.
“Hatua hiyo ya Mhe Mbunge wetu kufanya ziara zake na kutembelea maeneo mbalimbali ni jambo la kupongezwa kwani atakuwa anatoa mrejesho kwa wapiga kura wake,” amesema Jororo.
Hivi sasa kwenye mitandao ya kijamii ya magurupu ya Whatsapp Wilayani Simanjiro, baadhi ya watu wamekuwa wanahoji mbunge huyo kutofanya ziara ya kuwatembelea wananchi baada ya kutoka Bungeni jijini Dodoma.
“Mbunge amekuwa anonekana kwenye ziara za viongozi wengine wanapokuja Simanjiro hivyo anaonekana kuwa anadandia ziara za viongozi wenzake badala ya kufanya ziara zake mwenyewe,” amesema mmoja kati ya vijana hao.
Amesema hivi karibuni Waziri wa Madini Dotto Biteko alifanya ziara Mirerani na Ole Sendeka akaonekana hapo, huwezi kuita hiyo ni ziara ya Mbunge au anahofia hawezi kupata watu wengi?
“Juzi RC Manyara Mhe Queen Cuthbert Sendiga amefanya ziara Kata ya Naisinyai, Mhe Mbunge Ole Sendeka naye akadandia akatembelea shule ya sekondari Naisinyai na juzi kule Nakweni kwenye makabidhiano ya zahanati yaani watu hadi wamemsahau kumtaja kwenye shukrani, sababu hafanyi ziara zake za ubunge.
Amesema hatua ya mbunge huyo kuanza ziara zake mwenyewe itakuwa ni vyema kwani Serikali huwa inamuwezesha fedha za ziara mbunge wa Jimbo ila kwa Simanjiro hawamuoni zaidi ya kwenye sherehe za kimila na uzinduzi wa kwaya.
Amesema Ole Sendeka anafanya kazi zake Simanjiro kwa wakati mgumu kwani ofisi ya mbunge kila wakati imefungwa, hana katibu wa mbunge kisha hafanyi ziara za kutembelea wananchi.