Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amoni Mpanju, akizungumza wakati akifungua Mkutano wa kitaifa wa wadau wa Malezi na kutokomeza ukatili dhidi ya watoto,uliofanyika leo Julai 13, 2023 Jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake Makundi Maalum Sebastian Kitiku ,akielezea lengo la Mkutano wa kitaifa wa wadau wa Malezi na kutokomeza ukatili dhidi ya watoto,uliofanyika leo Julai 13, 2023 Jijini Dodoma,
Mtaalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya binadamu(NIMRI) ambaye pia ni mtafiti wa Malezi na kupinga ukatili dhidi ya watoto Dkt. Joyce Wamoyi akiwasilisha mada wakati wa mkutano wa taifa wa wadau wa Malezi na kutokomeza ukatili dhidi ya watoto, Julai 13, 2023 Jijini Dodoma.
Baadhi ya Wadau wa malezi na kutokomeza ukatili dhidi ya watoto nchini wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Taifa wa wadau hao, Julai 13, 2023 Jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amoni Mpanju,amewataka Viongozi wa Dini pamoja na wasimaminzi wa ndoa nchini kutoa elimu ya malezi ya Mtoto kwa wanandoa kipindi cha uchumba ili kupunguza ukatili unatokea kwa asilimia 60 ndani ya familia.
Wakili Mpanju ameyasema hayo leo Julai 13,2023 jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Taifa wa Wadau wa Malezi na kutokomeza ukatili dhidi ya watoto.
Mpanju amesema ukosefu wa elimu sahihi ya malezi na makuzi kwa wazazi na walezi hasa kwa watoto wa kiume ni miongoni mwa sababu zinazochochea mmomonyoko mkubwa wa maadili kwa watoto na vijana nchini.
‘’Haiwezekani tunaviongozi wa Dini wanafungisha ndoa, sasa kama tumewapa leseni ya kufungisha ndoa basi kwenye uchumba wawaandae vizuri wajue siyo kwenye ndoa wanaenda kustarehe tendo la ngono , wawaandae ili wajue majukumuu yao, hili ni jukumu la viongozi wa dini na wakimila, siyo wanafungisha ndoa wanaitupia serikali mzigo , je misingi ya kuwapata hawa wasiaminzi wa ndoa inafuatwa , siku hizi unamtafuta mtu kisa ni mweupe mnaenda basi anakuwa msimaminzi wakati huo yeye mwenyewe ndoa yake inamshinda atakujaje kusimamia yakwangu,’’ amesema wakili Mpanju.
Hata hivyo amesema ipo haja kwa wazazi na walezi kuja na mfumo mzuri wa malezi wenye kushinikiza uwajibikaji wa baba na mama katika kuboresha malezi na ulinzi wa watoto.
“Kwa mujibu wa Taarifa ya Makosa ya Ukatili wa Kijinsia na Unyanyasaji za Jeshi la Polisi kwa watoto kwenye kipindi cha Januari hadi Disemba, 2022 kulikuwa na matukio 12,163 (Wavulana 2,201 na Wasichana 9,962 nchini. Matukio yaliyoongoza ni Ubakaji (6,335), ulawiti (1,557) na Mimba za utotoni matukio (1,555).amesema Mpanju na kuongeza
“Serikali inathamini sana watoto kwa kutambua ndiyo rasilimali muhimu kwa ujenzi wa Taifa, hivyo imekuwa ikichukua hatua za makusudi kudhibiti vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na kukuza maadili kwenye familia na jamii” Amefafanua Mpanju.
Aidha wakili Mpanju amewataka wadau wanaotekeleza afua za malezi dhidi ya Mtoto kushirikiana na Tamisemi hasa katika ngazi ya halmashauri ili kuandaa mkakati wa Ulinzi na malezi kwa mtoto na kuona namna zitakavyotatuliwa.
Naye Mkurugenzi wa idara ya Maendeleo ya Mtoto Sebastian Kitiku amesema, jamii inahitaji tafiti za mara kwa mara ili kujua maeneo ambayo yanatakiwa kutiliwa mkazo kwenye masuala ya malezi na makuzi ya Mtoto yanayozingatia shahidi na afua za kisayansi
”Changamoto za malezi zipo nyingi na moja ya sababu zinazopelekea ni mwingiliano wa mila na desturi za jamii mbali mbali, na maendeleo ya teknolojia ya Habari.”amesema Bw.Kitiku
Akizungumza kwa niaba ya ISC, NIMRI na vyuo vikuu vya Oxford na CapeTown Mkurugenzi wa ICS Tanzania Kudely Sokoine amesema wameshirikiana kwa pamoja kuekeleza ajenda hiyo na mpango wa kujenga mazingira wezeshi ya kisera ili kuongeza na kupanua wigo wa utekelezaji wa Afua za malezi unaozingatia ushahidi wa kisayansi ili kupunguza ukatili dhidi ya wanawake na watoto
“Malengo Mahususi na Maalum ya mpango huu nikufanya upembuzi kuangalia sera za Tanzania katika masuala ya malezi, aidhaa tumejaribu pia kuangalua afua zinazotekelezwa na wadau, Mpango huu unaunga mkono jitihada za Viongozi wa Tanzia akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na wadau wengine.”amesema Kudely