Mbunge wa viti maalum mkoani Ruvuma Mariam Nyoka kulia,akikabidhi funguo ya Pikipiki kwa mkazi wa kijiji cha Mkapundwa Hamis Rashid Baba mwenye watoto mapacha watatu ili iweze kumsaidia katika malezi ya watoto wake.
Mkazi wa kijiji cha Mkapunda wilayani Tunduru Hamis Rashid kushoto,akipokea kofia ngumu ya kuendeshea Pikipiki kutoka kwa Mbunge wa viti maalum mkoani Ruvuma Mariam nyoka aliyewapatia pikipiki familia ya Rashid yenye watoto mapacha watatu ili iweze kuwaingizia kipato kwa ajili ya kulea na kuwatunza watoto wao.
Hamis Rashid na mkewe Judith Sichawe wakijaribu kuendesha Pikipiki iliyotolewa na Mbunge wa Viti maalum mkoa wa Ruvuma Mariam Nyoka ili iwaingizie kipato na kuwasaidia katika kulea watoto wao mapacha watatu.
Hamis Rashid kulia na mkewe Mwalimu Judith Sichawe katikati na watoto wao mapacha watatu wakiwa na furaha baada ya kupokea msaada wa Pikipiki kutoka kwa Mbunge wa viti maalum mkoa wa Ruvuma Mariam Nyoka(hayupo pichani)ili iwasaidie kuwaingizia kipato na matunzo ya watoto wao.
Na Muhidin Amri,
Tunduru
MBUNGE wa viti maalum mkoa wa Ruvuma Mariam Nyoka,ametoa msaada wa pikipiki yenye thamani ya Sh.milioni 2.5 kwa familia yenye mapacha watatu inayoishi kijiji cha Mkapunda wilayani Tunduru ili iwaingizie kipato kitakachosaidia kwenye malezi ya watoto wao.
Baba wa watoto hao Hamis Shaibu alisema,baada ya kujaliwa kupata watoto mapacha wanne alilazimika kumuomba Mbunge pikipiki ili iwasaidie kulea watoto kwa kubeba abiria kutokana na changamoto ya maisha waliyonayo.
Alisema hana kazi wala shughuli yoyote ya kumuingizia kipato,jambo ambalo lingeweza kumsumbua katika malezi ya watoto wake hasa ikizingatiwa kwamba yeye ndiyo kichwa cha familia licha ya mama wa watoto hao Judith Sichawe ni Mwalimu wa shule ya msingi.
Amemshukuru Mbunge kutokana na msaada huo,na kuhaidi kutumia pikipiki hiyo kufanyia biashara itakayowaingizia kipato ambacho kitakwenda kupunguza ukali na ugumu wa maisha kwenye safari ya malezi kwa watoto wao.
Aidha,amewaomba wasamaria wengine kuendelea kuwasaidia katika malezi na matunzo ya vijana wao kwa kutoa walichanacho kwa sababu watoto hao bado wana uhitaji wa vitu vingi.
Naye mama wa watoto Judith Sichawe alisema,alifanikiwa kujifungua mapacha wanne hata hivyo kwa bahati mbaya mtoto mmoja amefariki Dunia tangu mwezi Septemba mwaka jana na sasa wamebaki watatu wenye umri wa mwaka mmoja na miezi 2.
Mbunge wa viti maalum Mariam Nyoka alisema,amelazimika kutoa msaada huo kwa kuwa anatambua ugumu wa kulea na kutunza watoto mapacha kwa wakati mmoja na changamoto ya kimaisha inayoikabili familia hiyo.
Alisema,hiyo ni mara ya pili kuitembelea na kutoa msaada kwa familia hiyo yenye jukumu kubwa la kulea watoto wao hadi pale watakapokuwa watu wazima na kuanza kujitegemea.
Kwa mujibu wa Nyoka,kulea watoto mapacha watatu ni kazi ngumu inayohitaji kipato kikubwa,na yeye kama sehemu ya jamii ameona ni vyema kuisaidia familia hiyo pikipiki ambayo itakuwa chanzo kikubwa cha kuwaingizia kipato.
MWISHO.
Na Muhidin Amri,
Tunduru
MKUU wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro amesema,wamekamata zaidi ya ng’omba 800 waliovamia mashamba na kuharibu mazao ya wakulima katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Amesema,ng’ombe hao wamekamatwa kutokana na doria na operesheni kubwa inayoendelea ya kuwaondoa wafugaji wote wanaofanya ufugaji na kuingiza mifugo kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kisheria.
Mtatiro amesema hayo jana wakati akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake,na kusisitiza kuwa ni lazima wafugaji wote kwenda katika maeneo(vitalu)vilivyotengwa kwa ajili kufugia mifugo badala ya kuendelea na ufugaji holela.
“kuna tabia ya baadhi ya wafugaji kupeleka kwa makusudi mifugo yao kwenye mashamba na kuharibu mazao ya wakulima jambo linalosababisha migogoro mikubwa kati ya wakulima na wafugaji hao”alisema.
Kwa mujibu wa Mtatiro,serikali itaendelea kufanya doria na operesheni ya kuwaondoa wafugaji wote waliovamia kwenye maeneo yasiyoruhusiwa na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa vikosi vinavyofanya kazi ya kuondoa mifugo katika vijiji vyao.
Alisema,mwaka 2019 serikali wilayani Tunduru ilitenga jumla ya vitalu 250 ili vitumike kwa ajili ya ufugaji,hata hivyo ni vitalu 125 tu vimelipiwa na kutumika kwa ajili ya kazi hiyo.
Katika hatua nyingine Mkuu wa wilaya alisema,wamemkamata Afisa mtendaji wa kijiji cha Machemba na Misechela na wenyeviti wa vijiji hivyo,kwa kuruhusu wafugaji kuingiza mifugo kwenye maeneo ambayo hayakutengwa kwa ajili ya ufugaji.
Baadhi ya wananchi wa kata ya Namasakata wilayani humo wamesema,kata hiyo hakuna vitalu vya mifugo vilivyotengwa kwa ajili ya ufugaji, lakini kuna makundi makubwa ya mifugo.
Diwani wa kata hiyo Rashid Usanje alisema,makundi ya mifugo yanavamia mashamba na kuharibu mazao mashambani na kuiomba Serikali kuchukua hatua kuwadhibiti wafugaji na mifugo yao.