Waziri wa Habari,Vijana ,Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa ufafanuzi kuhusiana na taarifa iliyosambaa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii inayotokana na kauli ya Katibu MStendaji Baraza la Sanaa,Sensa ya Filamu na Utamaduni (BASFU) Dkt. Omar Salim Adam aliyoitoa Julia 11,2023 katika kipindi cha “Asubuhi njema ” kilochorushwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar ZBC kuhusiana na kutolewa kibali kwa Mwanamme yoyote anaetaka kusuka nywele,hafla iliyofanyika Wizara ya Habari Migombani Mjini Unguja julai 12,2023.PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO ZANZIBAR
Na Sheha Haji Sheha na Raima Mohamed Maelezo
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka faini ya shilingi milioni moja kwa mwanamme yeyote atakaesuka nywele.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe Tabia Maulid Mwita wakati akitoa ufafanuzi juu ya kauli iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa, Filamu na Sensa (BASFU) Zanzibar aliyotoa siku ya Jumanne July 11 katika kipindi cha Asubuhi njema kinachoshurushwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).
Amesema hakuna sheria ya kutoa kibali cha mwanamme yeyote anaetaka kusuka nywele bali ni kutoa faini ya hatia ya kosa hilo.
Waziri Tabia amefafanua kuwa Baraza la Sanaa Sensa na filamu na Utamaduni halina mamlaka ya kutoa kibali cha kusuka nywele na mambo kama hayo ni kinyume cha maadili, mila, silka na Utamaduni wa kizanibar.
Ameeleza kuwa Katibu Mtendaji pamoja na maelezo yote aliyoyaeleza yalikuwa na lengo la kutoa elimu kwa jamii juu ya namna bora ya kulinda silka na utamaduni wa Mzanzibari .
“Nakiri hapa kupitia vyombo vya habari kwamba Katibu Mtendaji aliteleza kwa kutoa kauli ya kwamba mwanamme yoyote Zanzibar anayetaka kusuka akate kibali cha shilingi milioni moja” alieleza Waziri.
Amesema Baraza la Sanaa kupitia watendaji wake wanatekeleza majukumu yao na kuhakikisha mila, silka na Utamaduni wa kizanibari unalindwa kwa mujibu wa kifungu cha 7(b) cha sheria namba 7 ya mwaka 2015.
Aidha, amefahamisha kuwa mambo ambayo yanavunja maadili ni wanaume wa kizanzibari kusuka kufanya hivyo ni kwenda kinyume na utamduni na atakaebainika atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kutozwa faini au kufungwa kifungo cha miezi sita.
Waziri Tabia ameomba radhi kwa kauli Karibu wa Baraza la Sanaa aliyoitoa katika kipindi cha Asubuhi Njema ameitoa kimakosa na sio kiutashi bali amekusudia kuielimisha jamii katika kufuata maadili ya nchi.
Aidha Waziri amesema Wizara bado inajukumu la kulinda Utamaduni wa kizanibari na kuheshimu tamaduni za watu wengine kwa kuzingatia haki za binadamu.
Amewataka wananchi wa Zanzibar kuendelea kulinda mila na Utamaduni kuongeza kutoa elimu kwa jamii kupitia njia mbalimbali ili kuzuia mmonyoko wa maadili nchini.