Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mheshimiwa Aswege Kaminyonge amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali katika Wilaya hiyo kuunga mkono na kuendeleza jitihada zinazofanywa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) za kuelimisha na kuhamasisha wananchi wa vijijini waliofikiwa na miundombinu ya umeme, kuchangamkia fursa kwa kuunganisha nishati hiyo na kuitumia kujiletea maendeleo.
Akizungumza katika vijiji mbalimbali wakati wa uhamasishaji, Msimamizi Miradi wa REA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Ernest Makale alisema azma ya Serikali siyo tu kuwafikishia nishati bora wananchi wa vijijini bali pia kuhakikisha wanazitumia kwa lengo la kuboresha maisha yao na ya Taifa kwa ujumla.
Mhandisi Makale amewahamasisha wananchi kutumia kipindi hiki cha mavuno kutenga fedha kwa ajili ya kufanya usambazaji wa nyaya (wiring) katika nyumba zao na kuvuta umeme ili waweze kufanya maendeleo mbalimbali na kujiajiri.
“Gharama za kufanya usambazi wa nyaya ndani ya nyumba (wiring) haizidi laki mbili. Lakini hata wale wafugaji wakiuza mbuzi au kondoo wanaweza kufanya usambazaji wa nyaya ndani ya nyumba zao na kuvuta umeme,” alisema Mhandisi Makale.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja Tanesco Mkoa wa Simiyu, Jimmy Jeremia amewasisitiza wananchi kutunza pamoja na kulinda miundombinu ya umeme kama nguzo pamoja na transfoma kwa kutochoma moto mashamba ambayo nguzo za umeme zinakatisha.