Sehemu ya majengo ya shule mpya ya msingi Kipera Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ambayo serikali imetoa shilingi milioni 513 kupitia mradi wa uboreshaji miundombinu ya shule za msingi (BOOST) kujenga madarasa 16,matundu ya vyoo 18 na jengo moja la utawala
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akitoa maelekezo kwa Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Kipera Silvester Nanguka baada ya kukagua ujenzi wa shule hiyo mpya ya msingi
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akitoa maagizo uongozi wa Manispaa ya Songea baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa shule mpya ya msingi Kipera.
Na Albano Midelo,Songea
SERIKALI imetoa shilingi milioni 893 kupitia mradi wa uboreshaji miundombinu ya shule za msingi (BOOST) katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Dkt.Frederick Sagamiko wakati anatoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya BOOST kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas alipofanya ziara ya siku moja ya kukagua miradi hiyo.
Amesema fedha hizo zinatumika kutekeleza miradi ya BOOST katika shule saba za msingi ambazo amezitaja kuwa ni Kipera, Amani, Mbulani, Matogoro,Bombambili,Mkuzo na Ruhuwiko na kwamba utekelezaji wa mradi umeanza Mei 15,2023 na miradi yote imefikia hatua ya ukamilishaji.
Dkt.Sagamiko amesema kati ya fedha hizo,shilingi milioni 513 zinajenga shule mpya ya msingi Kipera katika Kata ya Ruvuma yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 800 ambapo mradi unahusisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 16,matundu 18 ya vyoo na jengo la utawala.
“Shule ya msingi Amani imepokea shilingi milioni 66.3 kujenga madarasa mawili ya awali ya mfano,shule ya Mbulani milioni 77.1 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na shule ya Ruhuwiko milioni 77.1 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa,tunamshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kutujengea miundombinu bora ya shule za msingi’’,alisema.
Shule nyingine zilizopokea fedha za BOOST amezitaja kuwa ni Matogoro,Bombambili na Mkuzo ambazo kila shule imepokea milioni 53.1 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa.
Akizungumza baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa shule mpya ya msingi Kipera na ujenzi wa madarasa matatu katika shule ya msingi Ruhuwiko,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ameupongeza uongozi wa Halmashauri hiyo kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa mradi huo.
“Marekebisho yale madogo madogo yaliyoonekana yarekebishwe,kwa ujumla miradi inakwenda vizuri hongereni sana,fundi aongeze kasi ili mradi ukamilike kwa wakati,hakikisheni shule hii mpya ya msingi Kipera iwe ya mfano katika Mkoa wa Ruvuma’’,alisisitiza.
Ameagiza shule hiyo iwe na mazingira ya kuvutia yaliyopandwa maua,miti na bustani sanjari na kutengeneza njia za kupita wanafunzi hali ambayo itaweka mazingira rafiki ya kujifunza na kufundishia kwa walimu na wanafunzi.
Hata hivyo Kanali Thomas ametoa rai kwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Mheshimiwa Michael Mbano kuwaalika madiwani katika Halmashauri nyingine kufika katika Manispaa hiyo ili kujifunza namna ya kusimamia vizuri utekelezaji wa miradi.