Kaimu Mkuu wa Wilaya hiyo Martha Tevely ambaye ni Afisa Tarafa ya Manonga akizungumza na wananachi waliohudhuria mkutano huo wa kumaliza mgogoro kati ya miliki wa Leseni za madini na mwenye shamba .
Na Lucas Raphael,Tabora
MKUU wa Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora amefanikiwa kusuluhisha mgogoro wa shamba lenye madini ya dhahabu linalomilikiwa na familia ya Lemi John katika kijiji cha Mwamapuli, kata ya Kinungu wilayani humo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana kijijini hapo na kuhudhuriwa na pande 2 zinazohusika na mgogoro huo, Kaimu Mkuu wa Wilaya hiyo Martha Tevely ambaye ni Afisa Tarafa ya Manonga alisema pande zote zimeafikiana ili kumaliza ugomvi wao.
Alisema kabla ya mkutano huo Afisa Madini wa Mkoa na Afisa Ardhi wa Wilaya walipita kwenye shamba lenye mgogoro na kukutana na wanafamilia na Mwekezaji ili kujiridhisha kama malalamiko yanayosemwa yana ukweli wowote.
Alibainisha kuwa baada ya kutembelea mipaka ya shamba hilo na kujionea eneo alilopewa mwekezaji, walibaini kuwa mwekezaji kapewa eneo dogo tu la uchimbaji na sio kumilikishwa shamba lote.
‘Leseni iliyotolewa haimruhusu mwekezaji kufanya shughuli zake katika shamba lote linalomilikiwa na mama huyo kama video iliyorushwa mitandaoni inavyoeleza, hiyo ni clip ya uchochezi na upotoshaji’, alisema.
Kaimu DC alieleza kuwa sintofahamu hiyo sasa imeisha baada ya kuafikiana kuwa mwekezaji atalipa fidia kwa sehemu ya shamba atakalofanyia shughuli zake za uchimbaji na pia atalipa asilimia 10 ya mapato yake ya uchimbaji.
Alibainisha kuwa licha ya wanafamilia kupeleka suala hilo mahakamani, dhamira yake ni kuendelea kudumishwa amani na utulivu katika kijiji hicho na kata nzima huku akimtaka mwekezaji kuendelea kutekeleza makubaliano hayo kwa dhati.
Afisa Madini wa Mkoa huo Mhandisi Abel Madaha alisema kazi yao ni kusimamia sekta ya madini, kutoa leseni, kusimamia uchimbaji na kukusanya maduhuri na mwekezaji yeyote anayepewa leseni ni lazima azingatie sheria na taratibu zote.
Alisema awali waliafikiana baadhi ya mambo lakini baadae wakakiuka makubaliano yao hivyo akalazimika kusitisha shughuli za uchimbaji dhahabu katika eneo hilo ila baada ya kuweka sawa mambo yao waliruhusiwa kuendelea.
Alibainisha kuwa baadhi ya madalali (third part) wamekuwa chanzo kikubwa cha kuvuruga makubaliano baina ya pande 2 hivyo akaonya kuwa hawako tayari kuona mwekezaji akinyanyaswa bali apewe ushirikiano ili kuleta tija kubwa.
Mhandisi Madaha alisema mgogoro katika eneo hilo ulishaisha kinachotakiwa ni kuendelea kutoa elimu ya shughuli za uchimbaji madini kwa wananchi ili kuepusha upotoshaji.
Naye Afisa Ardhi wa wilaya hiyo Mussa Nkindwa alisema sheria ya ardhi iko wazi, mwekezaji yeyote anapotaka kuwekeza eneo linalomilikiwa na mwingine anapaswa kulipa fidia kwanza kabla ya kufanya kitu chochote kile.
Alibainisha kuwa sintofahamu hii imeibuka baada ya pande 2 kutoafikiana juu ya malipo na mwekezaji kuanza shughuli zake kabla ya kumalizana na mwenzake, taratibu na sheria ni lazima zizingatiwe huku akionya waopotoshaji .
Diwani wa kata hiyo Jolad Simon alipongeza serikali kwa kukutanisha pande zote 2 ili kufikia mwafaka mzuri wa kumaliza mgogoro huo kwa manufaa ya wanafamilia na mwekezaji, aliomba elimu ya shughuli za uchimbaji madini kuendelea kutolewa kwa wananchi wote.