Katibu Tawala Mkoa wa Singida (RAS) Dk. Fatuma Mganga akizungumza kwenye kikao kazi kilichofanyika Juni 23, 2023 cha wadau wa elimu cha kuweka mikakati ya kimkoa ya kuwalinda watoto shuleni dhidi ya vitendo vya ukatili.
Na Dotto Mwaibale,
Singida
KATIBU Tawala Mkoa
wa Singida (RAS) Dk. Fatuma Mganga ameagiza kufungwa kwa kamera za usalama
(CCTv Camera) katika shule ili kukomesha vitendo vya ukatili kwa watoto.
Dk.Mganga ametoa
maagizo haya Juni, 23, 2023 wakati akizungumza kwenye kikao kazi cha wadau wa
elimu cha kuweka mikakati ya kimkoa ya kuwalinda watoto shuleni dhidi ya
vitendo vya ukatili.
“Matumizi ya
teknolojia za kamera za usalama katika shule zetu zikiwekwa katika kila kona na
kwenye magari ya kuwabeba wanafunzi zitasaidia kuonesha vitendo hivyo na kupata
ushahidi wa moja kwa moja na kutokomeza ukatili wa aina zote hasa kwa
watoto,” alisema Mganga.
Aidha, Dk.Mganga
aliomba kuanzishwa kwa madawati ya ulinzi na usalama kwa mtoto mashuleni jambo
litakalo wafanya kuondoa woga wa kutoa taarifa za ukatili.
“Niwaagize
maafisa elimu wote kuhakikisha shule zote zinakuwa na madawati ya ulinzi na
usalama ili watoto waweze kujadili masuala ya ukatili na kutoa taarifa,”
alisema.
Alisema Serikali ya
Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza sana kwenye
miundombinu ya elimu ili kumsaidia mtoto wa kitanzania kupata elimu bure na
bora hivyo ni jukumu la watendaji kusimamia watoto wasifanyiwe vitendo hivyo
vya udhalilishaji.
Katika hatua
nyingine Dk.Mganga alitoa rai kwa viongozi wa sekta ya elimu mkoani hapa katika
shule zote za msingi na sekondari watoto wafundishwe kupitia wimbo wa ‘Don’t
Touch kampeni’ ulioasisiwa na Mkaguzi wa Polisi, Francis Msuku wa Kata ya
Gambushi, Bariadi mkoani Simiyu na kupongezwa na Rais Samia ili waelewe jinsi
ya kuzuia ukatili dhidi yao.
Ili kukabiliana na
vitendo hivyo vya ukatili dhidi ya watoto na kufikia malengo yanayohitajika Dk.
Mganga aliwataka maafisa ustawi na maendeleo ya jamii kutoka ofisini na kwenda kwa wananchi kutoa
elimu kuhusu haki na wajibu wao katika kumlinda mtoto na kuwaelekeza vizuri ni
wapi pa kukimbilia ili kupata huduma zinazostahili.
Pia Dk. Mganga
aliagiza urasimu katika utoaji huduma uondolewe kabisa ili kuleta imani kwa
wananchi kuhusu vyombo vyao vya dola.
Mganga Mkuu wa Mkoa
wa Singida, Victorina Ludovick alisema jitihada mbalimbali zimeendelea
kufanyika kwa kushirikiana na wadau na
wataalam wa maendeleo kwa kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari na
kutoa huduma za afya, unasihi,kisheria kwawahanga wa ukatili wa kijinsia na ukatili
dhidi ya watoto.