Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo ameahidi kurejesha Shilingi Milioni 228 iliyoelekezwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bahi ambayo
ilirudishwa hazina baada ya mwaka wa fedha kuisha na kusema ni haki yao fedha hiyo na itarudi kwa maendeleo ya Hospitali.
Chongolo ametoa ahadi hiyo alipokagua Hospitali ya Wilaya ya Bahi ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukagua Uhai wa Chama na Utekelezaji wa Ilani ya CCM Katika Mkoa wa Dodoma ambapo ameambatana na Katibu wa NEC-Oganaizesheni Issa Haji Gavu na Katibu wa NEC-Itikadi na Uenezi Sophia Mjema.
Akizungumza Hospitalini hapo, amesema fedha hizo zimechukuliwa
kimakosa na atazungumza na Waziri wa Fedha kuhakikisha Fedha hizo zinarudishwa na kutatua changamoto nyingine zilizopo katika Hospitali
hiyo.
Pia amesema tayari wamshatoa maelekezo kwa Wizara ya Fedha kuhakikisha Fedha zote ambazo zimeelekezwa kwenye Halmashauri kwa ajili ya Miradi kutorudishwa hazina bali ziendelee kutumika katika miradi hiyo kwa utaratibu maalumu ikiwemo kuandika maelezo.
Awali akitoa taarifa kwa Katibu Mkuu, Mganga Mfawadhi wa Hospitali ya Bahi amesema Hospitali hiyo imeanza kutoa huduma mwaka 2020 ikiwa na majengo saba.