Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. David Silinde akifungua mafunzo yenye Kauli Mbiu ya “Youth Bussiness Engangement Through Livestock” kwa vijana wajasiriamali wanaonenepesha mifugo kupitia vituo atamizi, Kampasi ya LITA Kikulula, wilayani Karagwe mkoa wa Kagera. Mhe. Silinde amewataka vijana wanufaika wa mpango huo kuwa wavumilivu, wasikivu na wadadisi zaidi ili kuweza kuzijua fursa mbalimbali zinazopatikana katika taasisi za fedha pamoja na asasi nyingine za maendeleo.
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Mhe. Julius Laizer akitoa akiwasalimu washiriki wa Mafunzo Atamizi kabla ya ufunguzi wa mafunzo yenye Kauli Mbiu ya “Youth Bussiness Engangement Through Livestock” kwa vijana hao waliopo kwenye Kampasi ya LITA Kikulula, wilayani Karagwe mkoa wa Kagera.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene akitoa taarifa fupi kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi kuhusu utekelezaji wa program ya Jenga Kesho iliyobora kwa vijana kupitia miradi ya ufugaji mifugo kibiashara wakati ufunguzi wa mafunzo yenye Kauli Mbiu ya “Youth Bussiness Engangement Through Livestock” yaliyoandaliwa kwa ajili ya vijana hao waliopo kwenye Kampasi ya LITA Kikulula, wilayani Karagwe mkoa wa Kagera.
Mshiriki wa Mafunzo Atamizi katika Kampasi ya Kikulula, Resti Mgonja (kulia) akisoma risala kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. David Silinde (wa pili kutoka kulia) wakati alipotembelea moja ya eneo wanalotumia kufugia mifugo yao. Kutoka kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene akifuatiwa na Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Mhe. Julius Laizer.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. David Silinde (wa sita kutoka kushoto mstari wa mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi, Wataalam na washiriki wa mafunzo yenye Kauli Mbiu ya “Youth Bussiness Engangement Through Livestock” kwa vijana wajasiriamali wanaonenepesha mifugo kupitia vituo atamizi katika Kampasi ya LITA Kikulula, wilayani Karagwe mkoa wa Kagera mara baada ya kufungua mafunzo hayo
Na.Mwandishi Wetu.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. David Silinde amesema serikali inaendelea kutekeleza mpango wa kuhakikisha wafugaji wanafuga kisasa na kibiashara ili kuongeza tija kwa wafugaji na mchango wa Sekta ya Mifugo kwenye pato la taifa.
Silinde ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo yenye Kauli Mbiu ya “Youth Bussiness Engangement Through Livestock” kwa vijana wajasiriamali wanaonenepesha mifugo kupitia vituo atamizi, Kampasi ya LITA Kikulula, Karagwe.
Katika kufanikisha utekelezaji wa mpango huo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iliandaa mwongozo ambao umeainisha majukumu ya wadau mbalimbali walioko katika mnyororo wa thamani wa sekta ya mifugo. Kwa upande wa taasisi za fedha ikiwemo mabenki, Wizara, pamoja na mambo mengine, inawategemea kusaidia kubadilisha fikra na mitazamo ya vijana kuwa ya kibiashara ili kuweza kutengeneza fursa nyingi zaidi za ajira kupitia sekta ya mifugo; pamoja na kuwafundisha namna ya kuandaa mipango biashara kwa ajili ya kuanzisha au kuendeleza biashara zao mara baada ya kumaliza muda wao katika Vituo Atamizi.
“Nawapongeza LITA na Benki ya NMB kwa kutumia fursa hii kutoa mafunzo na kuwaandaa vijana wetu kikamilifu kuwa wawekezaji na wafanyabiashara watarajiwa. Kupitia mafunzo haya pia mnaendelea kuwandaa wateja wenu watarajiwa kupitia mikopo yenye riba na masharti nafuu. Naamni ninyi pamoja na wadau wengine mtaendelea kutoa mafunzo kama haya katika vituo vingine ambavyo viko chini ya Wizara yetu,” alisema Silinde
Silinde amewataka vijana kutokata tamaa kwa kuwa maisha ni mapambano hata pale watakapokutana na changamoto ya aina yoyote wanatakiwa kutafuta njia ya kukabiliana nayo na sio kukata tamaa. Vilevile amewataka vijana waliopata fursa ya kupatiwa mafunzo kuwa mfano katika kuleta taswira na dira mpya katika taifa kupitia Sekta ya Mifugo na Uvuvi.
Aidha, amewataka vijana wanufaika wa mpango huo kuwa wavumilivu, wasikivu na wadadisi zaidi ili kuweza kuzijua fursa mbalimbali zinazopatikana katika taasisi za fedha pamoja na asasi nyingine za maendeleo. Vijana wametakiwa kujituma zaidi ili kuweza kufikia ndoto na maono ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kuendelea kuongeza kipato na fursa za ajira kwa vijana na wanawake wengi wa hapa nchini.
Mtendaji wa Wakala ya Vyuo vya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia LITA na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) imeanza kutekeleza program ya Jenga Kesho iliyobora kwa vijana wetu kupitia miradi ya ufugaji mifugo kibiashara kupitia vituo atamizi nane (8) nchi nzima. Vituo hivi viko katika mkoa wa Tanga, Mwanza na Kagera. Tayari kuna washiriki 240 wamedahiliwa ambapo kila mshiriki atapata fursa ya kunenepesha ng’ombe wasiopungua 40 katika mizunguko minne ndani ya mwaka mmoja. Mzunguko wa kwanza wa unenepeshaji umeanza ambapo ng’ombe wapatao 2,400 wamenunuliwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Mhe. Julius Laizer ameishauri Wizara kuangalia uwezekano wa kutenga asilimia 20 ya maeneo ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kwa ajili ya kutumika na vijana kwa shughuli za ufugaji ili wanapomaliza mafunzo wasihangaike kutafuta ardhi kwa ajili ya kufugia.
Mshiriki wa Mafunzo Atamizi katika Kampasi ya LITA Kikulula, Resti Mgonja wakati akisoma risala amesema toka mafunzo hayo yameanza wamefanikiwa kupata elimu ya unenepeshaji kuanzia kwenye ushiriki wa ununuzi wa ng’ombe mnadani ambapo wamenunua ng’ombe 600, wamefanya uogeshaji wa ng’ombe ili kuwakinga na magonjwa, wamefanikiwa kuongeza uzito wa kilo 50 kwa ng’ombe ndani ya siku 90 na kufanikiwa kufyeka maeneo kwa ajili ya malisho takribani ekari 50.