Na. Damian Kunambi, Njombe
Baraza la madiwani wilayani Ludewa mkoani Njombe limeadhimia kutoendelea kumfumbia macho Mkandarasi wa ujenzi wa jengo la Utawala la Halmashauri ya wilaya hiyo na kumtaka mpaka ifikapo Julai 8 mwaka huu kuhakikisha ujenzi huo umekamilika kwa mujibu wa mkataba.
Maazimio hayo yamefanyika mara baada ya kuwasilishwa hoja ya ujenzi wa jengo hilo katika kikao maalum cha Baraza hilo la madiwani kilicholenga kujadili majibu ya hoja na mpango kazi wa utekelezaji wa hoja za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ambapo kwa mujibu wa taarifa ya hoja hiyo imeeleza kuwa jengo hilo limekuwa likisuasua kutokana na uchache wa vibarua waliopo.
Akizungumza kwa niaba ya Madiwani hao mwenyekiti wa halmashauri hiyo Wise mgina amesema ujenzi wa jengo hilo unatakiwa kumalizika kwa wakati na endapo itafika tarehe hiyo pasipo kukamilishwa ndipo watajua cha kufanya kulingana na mkataba wa mkandarasi huyo unavyo jieleza.
Amesema hata hivyo kamati ya mikopo na fedha ilishauri menejimenti kuzingatia maoni ya kamati ya ukaguzi wa kutaka jengo hili likamilike kwa wakati na kisha alitumia fursa hiyo kuliuliza baraza hilo endapo linaridhia hilo ambapo baraza hilo lilikubaliana na adhimio hilo.
Aidha kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Sunday Deogratias amesema mpaka sasa jengo hilo tayari limefikia hatua ya zaidi ya 75% na vifaa vyote vya kukamilisha hatua iliyobaki tayari vilisha nunuliwa.
“Tulishakaa na mkandarasi huyu na kuongea nae juu ya kukamilisha jengo hili kwa wakati ambapo tuliwekeana utaratibu na mkakati na kisha kukubaliana kuwa ifikapo tarehe hiyo 8 ya mwezi wa saba ujenzi huu uwe umekamilika kwakuwa vifaa vyote vipo”. Amesema Deogratias.