Na Mwamvua Mwinyi-Mkuranga
JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani imesema Jeshi la Polisi Wilaya ya Mkuranga imefanya kazi kubwa, kudhibiti vitendo vya uhalifu ambavyo vilikuwa vinatishia usalama wa wananchi.
Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Wazazi Kata ya Kitomondo, Mjumbe wa Baraza la Wazazi Mkoa ,Hamis Mtutu alisema kwa sasa hali ya kiusalama imeimarika na matukio ya uhalifu yamepungua.
Mtutu alieleza, kupitia kwa ofisa upelelezi wa Wilaya amepambana na hata mashauri yanapokwenda kwenye ofisi hiyo masuala hayo yanafanyiwa kazi kwa haraka.
“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uteuzi wa IGP Camilius Wambura ambae naye alimteua ofisa upelelezi wa Wilaya Jongo Ali ambapo mashauri ya kipelelezi yanafanyiwa kazi mapema hivyo kupunguza changamoto ya kulaza malalamiko,”alisema Mtutu.
Alieleza, matukio ya kihalifu yalikuwa ni mengi sana lakini kwa sasa hali imebadilika na kuwa ya utulivu na watu wanaishi kwa amani na utulivu.
Akizungumzia kuhusu maandalizi ya uchaguzi wa nafasi ya wenyeviti wa vijiji na vitongoji mwakani alisema kuwa ili CCM ifanye vizuri waondoe makundi.
Alibainisha, makundi siyo mazuri kwani kama wanaona kuna tatizo ndani ya chama wanapaswa kukaa na kuyaongea na si kukivuruga chama na kuleta makundi.
Nae Diwani wa Viti Maalum Shukuru Muyugi alieleza, changamoto kubwa kwenye kata hiyo ni ubovu wa barabara ambapo wanaamini yakifanyika maboresho na kuondoa changamoto hiyo mambo yatakuwa mazuri.
Awali akisoma risala ya Juimuiya ya Wazazi Kata ya Kitomondo Katibu Rajabu Bungurumo alisema kuwa changamoto ni kutokamilika jengo lao hatua ya umaliziaji.
Bungurumo alisema kuwa changamoto ya barabara hivyo wananchi kushindwa kuwa na uhakika wa usafiri wa kutoka na kuingia kwenye kata hiyo.