Baadhi ya wafanyabiashara wa soko la Azimio wilayani Tunduru wakimsikiliza Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ambaye pia ni Mkuu wa wilaya hiyo Wakili Julius Mtatiro(hayupo pichani).
Mfanyabiashara wa soko la Azimio wilayani Tunduru Ali Bakari akieleza changamoto wanazokutananazo katika soko hilo ikiwemo vitendo vya wizi na huduma mbovu ya choo mbele ya Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro.
Zaitun Ahmad mfanyabiashara katika soko la Azimio mjini Tunduru akieleza changamoto ya huduma ya maji safi na salama katika soko hilo.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Wakili Julius Mtatiro, akizungumza na wafanyabiashara wa soko la Azimio katika mkutano wake wa kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara sokoni hapo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Tunduru Chiza Marando akitoa ufafanua juu ya kero na changamoto mbalimbali zilizopo katika soko la Azimio.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Wakili Julius Mtatiro, akitoa maelekezo kwa mwakilishi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Tunduru Joseph Buchele kuhusu kuboresha huduma ya maji katika soko la Azimio ambapo kwa sasa wafanyabiashara wa soko hilo wanalazimika kwenda mbali na maeneo yao kufuata huduma hiyo.
Na Muhidin Amri,
Tunduru
BAADHI ya wafanyabiashara katika soko la Azimio wilayani Tunduru,wamelalamikia kukithiri kwa vitendo vya wizi na udokozi wa bidhaa zao jambo linalorudisha nyuma jitihada za kujitafuta kipato na kukuza uchumi wa familia na Taifa.
Wakizungumza mbele ya Mkuu wa wilaya hiyo Wakili Julius Mtatiro walisema,vitendo hivyo vinafanywa na walinzi wanaoshirikiana na vibaka wanaoingia ndani ya soko na kuiba bidhaa mbalimbali.
Kassim Makasi alisema, matukio hayo yanatokea nyakati za usiku kwa kuwa mageti ya soko ni mabovu na baadhi ya walinzi waliowekwa na Halmashauri wanafika kazini wakiwa wamelewa na wengine wazee,hivyo ni rahisi vibaka kuingia ndani na kufanya uharifu jambo linalo wasababishia hasara kubwa.
“mara kwa mara mafundi wanakuja kuchukua vipimo kwa ajili ya kutengeneza mageti mapya lakini tunasikitika sana tangu mwaka jana hakuna kilichotekelezwa,tunakuomba Mkurugenzi weka mageti mapya ili yatusaidie ulinzi wa bidhaa zetu”alisema Makasi.
Aidha alisema,baadhi ya walinzi siyo waaminifu na wanahusika moja kwa moja kuiba bidhaa zao na kuiomba Halmashauri kuwafukuzwa katika soko hilo ili wapatikane walinzi wengine watakaosaidia kuimarisha ulinzi.
Ali Bakari, amelalamikia huduma mbovu ya vyoo kwani matundu yaliyokuwepo ni machache,na wanalazimika kwenda maeneo mengine nje ya soko kupata huduma hiyo.
Alisema soko hilo ni sehemu ya mapato kwa Halmashauri,hivyo ni muhimu serikali kuimarisha miundombinu yake badala ya kukimbilia kuchukua fedha za pango na ushuru kutoka kwa wafanyabiashara.
Zaitun Ahmad alisema,wafanyabiashara wa soko hilo wako katika hatari ya kupata magonjwa ya milipuko ikiwemo kipindu pindu,kuharisha na magonjwa ya tumbo kutokana na kukosekana kwa huduma ya maji safi na salama.
Mwenyekiti wa Chama cha wafanyabiashara wilayani Tunduru Efrem Mbwilo alisema,Halmashauri ya wilaya imepora baadhi ya vibanda vilivyojengwa na wafanyabiashara na kuwapa watu wengine.
Alisema kisheria vibanda hivyo ni vya Halmashauri,lakini vimejengwa na wafanyabiashara ambao ndiyo wamiliki halali kwa hiyo Halmashauri haikupaswa kuwapora,badala yake ilitakiwa kukaa nao ili kuingia makubaliano mapya.
“Halmashauri haijawahi kujenga vibanda katika soko hili,vibanda vyote vimejengwa na watu na wafanya biashara wamenunua kutoka kwa wamiliki wa awali”alisema Mbwilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Chiza Marando amekiri kuwepo kwa changamoto hizo na kueleza kuwa,kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri imetenga kiasi cha fedha zitakazotumika kufanya ukarabati wa soko na kuboresha huduma zake ikiwemo maji na vyoo.
Akizungumzia changamoto ya kukithiri kwa uchafu sokoni hapo alisema,tayari wamefanya matengenezo ya lori moja na kutenga fedha kwa ajili ya kununua lori jipya ambayo yatafanya kazi ya kuzoa taka siyo katika soko tu bali katika maeneo yote mji wa Tunduru.
Pia,amewataka wafanyabiashara kulipa kodi za vibanda kwa wakati ili kuepuka usumbufu au kulazimika kulipa faini kubwa.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro ametoa wiki mbili kwa Halmashauri ya wilaya kuhakikisha ina Imarisha ulinzi kwa kujenga mageti mapya na kuboresha huduma ya vyoo na maji katika soko hilo.
Alisema,malalamiko yote ya wafanyabiashara yana ukweli na kama Halmashauri itashindwa kutatua kero hizo kutokana na mamlaka aliyonayo anaweza kuamuru wafanya biashara wasilipe pango za vibanda wala ushuru kwa muda wa miezi sita ili fedha hizo zitumike kuimarisha ulinzi na huduma muhimu.