Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana Juni 10, 2023 Jijini Dar es Salaam amekabidhi Bendera kwa Timu ya Olimpiki Maalum inayokwenda Berlin Nchini Ujerumani kushiriki mashindano ya Dunia katika jiji la Berlin nchini Ujerumani kuanzia Juni 17 hadi 25 mwaka huu.
Na Shamimu Nyaki
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Wizara kupitia Baraza la Michezo Tanzania imegharamia tiketi 15 za ndege zenye thamani ya Shilingi Milioni 50 kwa timu ya Olimpiki Maalum inayokwenda kushiriki mashindano ya Dunia katika jiji la Berlin nchini Ujerumani kuanzia Juni 17 hadi 25 mwaka huu.
Mhe. Chana amesema hayo leo Juni 10, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akikabidhi Bendera kwa Timu hiyo inayokwenda kushiriki mashindano hayo akiwataja pia Wadau waliounga mkono safari hiyo ambao ni Bodi ya Special Olympic ambayo imetoa tiketi 8 za thamani ya Shilingi Milioni 26. 8 na Azam Media tiketi 2 za Milioni 6.7.
Wadau wengine ni Sibusiso Foundation Arusha ambao waligharamia Kambi ya Mazoezi Jijini Arusha na ASAS ambao wametoa fulana 50 zenye thamani ya Shilingi Milioni 1.2. Kufuatia michango hiyo, Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana amewashukuru wadau hao pamoja na kuwakaribisha wadau wengine waendelee kuunga mkono shughuli za michezo hapa nchini.
“Nawapongeza Viongozi wa Special Olympic Tanzania na Wadau wote ambao wamechangia kufanikisha maandalizi ya safari hii, nawatakia heri vijana wetu, nendeni mkaliwakilishe vyema Taifa letu, tuko nyuma yenu tunawaombea” amesema Mhe. Chana.
Michezo hiyo hufanyika kila baada ya miaka minne, ambapo mara ya mwisho imefanyika mwaka 2019, Abudhab Flame za Kiarabu, Tanzania ilishiriki katika mchezo wa Mpira wa Wavu na kuibuka mabingwa kwenye mchezo huo pamoja kupata medali ya Fedha kwenye mchezo wa Riadha.