Makamu Mwenyekiti wa Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii (SMAUJATA) Kata ya Manyoni mkoani Singida , Wallece Shechambo akitoa elimu ya kupinga ukatili wakati walipokuwa wakishiriki shughuli ya kijamii ya ujenzi wa madarasa katika Shule Mpya ya Msingi ya Muungano Maghorofani hivi karibuni, ambapo walizindua kampeni mpya ya kuongeza mashujaa wa kupinga ukatili ijulikanayo kama ‘Two by Two,
………………………………………….
Na Dotto Mwaibale, Manyoni
SHUJAA wa Maendeleo
na Ustawi wa Jamii (SMAUJATA) Kata ya Manyoni mkoani Singida wameanzisha
kampeni ya kuongeza mashujaa kwa kila nyumba kwa ajili ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia
ambayo itajulikana kwa jina la Wawili kwa Wawili (Two by Two).
Akizungumza na waandishi wa habari Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA wa kata
hiyo, Wallece Shechambo wakati walipokuwa wakishiriki shughuli ya kijamii ya ujenzi
wa madarasa katika Shule Mpya ya Msingi ya Muungano Maghorofani alisema kampeni
hiyo imelenga kuongeza mashujaa wa mapambano ya kutokomeza vitendo vya ukatili
katika kata hiyo na maeneo mengine yote ya wilaya ya Manyoni.
“Kampeni hii tumeipa jina la wawili kwa wawili ‘Two by Two’ yaani tutapita
kila kaya iliyopo ndani ya kata yetu kutoa elimu ya kupinga ukatili na
kuhamasisha watu wawili katika nyumba husika wawe mashujaa ambao nao watakwenda
kwenye kaya iliyo jirani nao kutafuta mashujaa wawili hadi kila nyumba iwe na
mashujaa hao,” alisema Shechambo.
Alisema kampeni hiyo itasaidia kuwa na mashujaa kila nyumba wa kupinga
ukatili na kuwa kama kata yao itakuwa na kaya 10,000 basi na mashujaa watakuwa
20,000 jambo litakalo saidia kutokomeza kabisa vitendo hivyo kama sio
kuvipunguza.
Shechambo alisema kampeni hiyo ya majaribio kama itafanikiwa wataisambaza
katika kata zingine na kuwa kila kiongozi wa SMAUJATA wa kata hiyo ametakiwa kuwa
wa kwanza kupita katika kila kaya kupata mashujaa hao wawili.
Alisema mashujaa watakao patikana kwenye kaya hizo wanaweza kuwa baba na
mama, wasichana au wavulana bila kujali
elimu na taaluma zao ili mradi tu waweze kupaza sauti ya kufichua vitendo vyote
vya ukatili na kutoa taarifa kwenye vyombo husika kama ofisi za kata na dawati
la jinsia lililopo katika vituo vya polisi na kwa maafisa ustawi wa jamii.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kitongoji cha Mwembeni, Saluthary Naaly alisema
moja ya kazi ya Mashujaa wa SMAUJATA ni kushiriki katika shughuli mbalimbali za
kijamii ambapo wataweza kukutana na wananchi na kuwapa elimu hiyo ya kupinga
ukatili.
Alisema kampeni hiyo ya Two by Two inakwenda kumaliza kabisa ukatili katika
kata hiyo na maeneo mengine kwa kuwa kila nyumba itakuwa na shujaa wa kupinga
vitendo hivyo.
Alisema kazi kubwa waliyoifanya wakati wakishiriki ujenzi wa shule hiyo ni
ubebaji wa matofali, kuchota maji na kutolewa kwa elimu ya kupinga vitendo vya
ukatili, madhara ya ndoa za utotoni na kuwanyima watoto haki ya kupata elimu
iliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA wa kata hiyo, Wallece Shechambo.
Katibu wa SMAUJATA wa kata hiyo Sarah Yohana alisema changamoto kubwa
iliyopo kwa baadhi ya wanaume ni kuwabana wake zao na kushindwa kushiriki katika mambo
mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali na
kupinga ukatili.
Makamu Katibu wa SMAUJATA wa kata hiyo, Joyce Peter alisema kuna faida
kubwa ya kushirikiana baina ya familia na familia katika shughuli mbalimbali
ziwe za huzuni, furaha na maendeleo jambo kubwa likiwa ni kudumisha upendo.
Mjumbe wa SMAUJATA wa kata hiyo, Neema Masabuni alizungumzia kuhusu madhara
yanayoweza kutokea kutokana na kutokuwepo kwa ushirikiano katika jamii na kuwa
siku zote utengano ni udhaifu.
Kwa upande wake Mjumbe wa SMAUJATA wa kata hiyo, Matilda Musa alizungumzia
kuhusu wajibu wa kuwa na uhusiano mzuri katika familia huku mjumbe mwenzake Zena
Salimu akihimiza suala zima la kufichua vitendo vya ukatili.
Mwenyekiti wa SMAUJATA wa Kata hiyo, Hussein Kheri alitumia nafasi hiyo
kuelezea umuhimu wa ujenzi wa shule hiyo na kuwa itasaidia kupunguza mlindukano
wa wanafunzi katika shule ya Mwembeni yenye watoto 1772 na watoto kusoma katika mazingira bora
ambapo aliipongeza Serikali chini ya Rais Dk.Samia Suluhu
Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa shule hiyo.