Na Jacquiline Mrisho
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kuwa idadi ya faru weusi imeendelea kuongezeka kutoka 163 mwaka 2019 hadi 238 mwaka 2022 na hivyo kuvuka lengo la Mkakati wa Kitaifa wa Kuhifadhi Faru 205 ifikapo Desemba 2023.
Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.
“Wizara imeendelea kuongeza jitihada za kuimairisha ulinzi na uhifadhi wa rasilimali za maliasili kwa kudhibiti ujangili, biashara haramu ya nyara, uvunaji haramu wa mazao ya misitu na nyuki na uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa ambapo jitihada hizo pamoja na mambo mengine zimewezesha kuongezeka kwa idadi ya Faru weusi kufikia 238 mwaka 2022”, alisema Mchengerwa.
Ameongeza kuwa, jitihada hizo zimeongeza idadi ya tembo kutoka 43,330 mwaka 2014 hadi 60,000 mwaka 2023 na kuifanya Tanzania kuendelea kuwa nchi ya tatu barani Afrika kwa kuwa na tembo wengi. Sambamba na hilo, taarifa za hali ya usalama zinaonesha katika kipindi cha mwezi Julai 2022 hadi Aprili 2023 hakuna vifo vya wanyamapori vilivyotokana na ujangili vilivyoripotiwa.
Aidha, ameendelea kusema kuwa Tanzania imeendelea kuongoza duniani kwa kuwa na simba wengi wapatao 14,912 na twiga 24,000 ambapo ongezeko hilo linathibitisha kupungua kwa ujangili wa wanyamapori nchini na linadhihirisha matokeo ya mipango bora na ushirikiano katika uhifadhi.
Vilevile ameeleza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na juhudi mbalimbali za Serikali ikiwa ni pamoja na kufanya siku doria 479,242 zilizowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa 12,058 pamoja na nyara mbalimbali za Serikali pia, Wizara imefanya operesheni maalumu za kiintelejensia zilizowezesha kuzuiwa kwa matukio ya ujangili na uvunaji haramu wa mazao ya misitu, kukamata silaha mbalimbali zikiwemo bunduki 214, risasi 1,427 na kuvunjwa kwa mitandao saba ya ujangili.
Sambamba na hilo, Wizara imeendelea kuimarisha Jeshi la Uhifadhi la Wanyamapori na Misitu kwa kutoa mafunzo ya ndani na nje ya kijeshi, upelelezi, uchunguzi na usimamizi wa kesi kwa askari wake kwa lengo la kuimarisha uhifadhi ambapo katika mafuzo hayo, jumla ya Askari 54 walishiriki.